Matendo Ya Mitume 27

Paulo Asafirishwa Kwenda Rumi

1Ilipoamuliwa kwamba twende Italia, walimkabidhi Paulo na wafungwa wengine kwa askari mmoja aitwaye Juliasi ambaye alikuwa wa kikosi cha Kaisari Agusto. Tulipakia meli iliyotoka Adrami tio ambayo ilikuwa ikielekea kwenye bandari zilizopo pwani ya Asia. Tukaanza safari yetu tukiongozana na Aristarko, Mmakedonia wa kutoka Thesalonike. Kesho yake tulifika Sidoni. Juliasi akamfanyia wema Paulo, akamruhusu aende kuwaona rafiki zake wam hudumie. Kutoka huko tuliendelea na safari yetu, na kwa kuwa tulikuwa tunakabili upepo, tukapitia upande wa kisiwa cha Kipro usioelekea upepo. Tukavuka bahari, kutoka upande wa Kilikia, na Pamfilia, tukafika Mira, katika jimbo la Likia. Yule askari akapata meli iliyokuwa inatoka Aleksandria ikielekea Italia, akatupakia humo. Tukasafiri pole pole kwa siku nyingi, na kwa shida na hatimaye tukafika karibu na bandari ya Nido. Lakini kwa kuwa upepo mkali ulikuwa ukivuma kutoka tulikokuwa tukielekea, hatukuweza kuendelea moja kwa moja na safari yetu, bali tulipitia upande wa pili wa Krete tukaizunguka ncha ya Salmone. Baada ya kuizunguka kwa shida tulifika sehemu iitwayo Bandari Nzuri, kar ibu na mji wa Lasea.

Tulikuwa tumepoteza muda mrefu baharini na kwa wakati huu safari ilikuwa ya hatari kwa maana majira ya kufunga yalikuwa yamekwisha pita. Paulo akawaonya marubani wa ile meli akasema, 10 ‘ ‘Mabwana, naona tukiendelea na safari hii patatokea maafa na hasara kubwa kwa meli na shehena na hata maisha yetu yatakuwa hatarini.” 11 Lakini yule askari akaamua kusikiliza zaidi ushauri wa nahodha na mwenye meli kuliko maneno ya Paulo. 12 Kwa kuwa ile bandari ilikuwa haifai kukaa wakati wa majira ya baridi, wengi wakashauri kwamba waendelee na safari na pengine kwa bahati wangeweza kufika Foinike. Hii ni bandari iliyoko katika kisiwa cha Krete na ambayo inatazama upande wa kusini-magharibi na kas kazini-magharibi, kwa hiyo wangeweza kukaa huko mpaka majira ya baridi yaishe.

Dhoruba Baharini

13 Upepo ulipoanza kuvuma taratibu toka kusini, wakadhani kuwa hii ilikuwa ni dalili nzuri kwamba wangeweza kuendelea na safari. Kwa hiyo wakang’oa nanga wakasafiri wakipita kando kando ya pwani ya kisiwa cha Krete. 14 Lakini baada ya muda mfupi upepo mkali uitwao ‘Kaskazi-mashariki’ ukavuma toka nchi kavu; 15 ukaipiga ile meli, na kwa kuwa haikuwa rahisi kushindana nao, tukaiachilia meli isukumwe kuelekea kule upepo unakokwenda. 16 Hatimaye tukasafiri kupitia nyuma ya kisiwa kidogo kiitwacho Kauda, ambapo kwa kuwa tulikuwa tumekingiwa upepo na hicho kisiwa, tuliweza kwa shida kuifunga mashua ya kuokolea watu. 17 Watu walipokwisha ivuta mashua hiyo wakaiingiza katika meli, waliifunga kwa kamba kwenye meli. Kisha, kwa kuogopa kwamba wangesukumwa na upepo mkali na kukwama kwenye mchanga karibu na pwani ya Sirti, walishusha matanga wakaiacha meli ielee. 18 Kesho yake dhoruba kali iliendelea kuvuma, kwa hiyo wakaanza kuitupa shehena baharini. 19 Siku ya tatu wakaanza kutupa vifaa vya meli baharini kwa mikono yao wenyewe. 20 Kwa siku nyingi hatukuona jua wala nyota, na dhoruba kali ilikuwa inaendelea kuvuma. Kwa hiyo tukakata tamaa kabisa kwamba tungeokolewa.

21 Kwa kuwa walikuwa wamekaa siku kadhaa bila kula cho chote, Paulo akasimama kati yao akasema, “Mngenisikiliza wala msingeondoka Krete na kupata mkasa huu na hasara hii. 22 Lakini sasa nawaomba mjipe moyo. Hakuna hata mmoja wenu atakayepoteza maisha yake ila meli hii itaangamia. 23 Jana usiku, malaika wa Mungu wangu ambaye mimi namwabudu alisimama karibu yangu 24 akasema, ‘Usiogope Paulo; huna budi kujitetea katika kesi yako mbele ya Kaisari; na kwa neema yake, Mungu amekupa maisha ya watu wote wanaosafiri pamoja na wewe.’ 25 Kwa hiyo muwe na matu maini kwa maana nina imani kwa Mungu kwamba mambo yatakuwa kama nilivyoambiwa. 26 Lakini hata hiyo meli yetu itakwama kwenye kisiwa fulani. ”

27 Siku ya kumi na nne, mnamo saa sita za usiku, tulipokuwa bado tunasukumwa na upepo katika bahari ya Adria, mabaharia wali hisi kwamba walikuwa wanakaribia nchi kavu. 28 Kwa hiyo wakapima kina cha bahari wakakuta kilikuwa mita thelathini na tano hivi, na baada ya kitambo kidogo wakapima tena wakapata kina cha mita ishirini na sita hivi. 29 Wakaogopa kwamba meli yetu ingegonga kwenye miamba, kwa hiyo wakashusha nanga nne nyuma ya meli, wakawa wanaomba kupambazuke. 30 Mabaharia walikuwa wanataka kutoroka kutoka mle melini, wakashusha mashua baharini wakidanga nya kuwa walikuwa wanakwenda kuweka nanga upande wa mbele ya meli. Ndipo 31 Paulo akawaambia wale maaskari na maofisa wao, “Hawa watu wasipobaki katika meli, hamtaweza kuokolewa.” 32 Basi wale askari wakakata kamba zilizoshikilia ile mashua kwenye meli wakaiacha mashua ichukuliwe baharini. 33 Mapambazuko yalipokaribia, Paulo akawasihi watu wote wale chakula akisema, “Leo ni siku ya kumi na nne mmekuwa katika wasiwasi bila kula cho chote. 34 Kwa hiyo nawasihi mle chakula kwa maana mnakihi taji ili muweze kuishi. Hakuna mmoja wenu atakayepoteza hata unywele mmoja kichwani mwake.” 35 Baada ya maneno haya, Paulo akachukua mkate, akamshukuru Mungu mbele yao wote, akaumega akaanza kula. 36 Ndipo wote wakatiwa moyo, wakaanza kula chak ula. 37 Ndani ya meli tulikuwa jumla ya watu mia mbili na sabini na sita. 38 Baada ya wote kula chakula cha kutosha, wakapunguza uzito wa meli kwa kutupa ngano baharini.

39 Kulipokucha, mabaharia hawakuitambua ile nchi, lakini waliona ghuba yenye ufuko wa mchanga ambako walitaka waielekeze meli kama ingewezekana, ili wafike pwani. 40 Kwa hiyo wakatupa nanga zote baharini, wakalegeza kamba zilizokuwa zikishikilia usukani wa meli, na kutweka tanga la mbele lishike upepo na kuisukuma meli kuelekea pwani. 41 Lakini ile meli ikagonga mwamba ikakwama kwenye mchanga na upande wa mbele wa meli uka banwa kwenye mwamba wala usingeweza kuondolewa tena. Na upande wa nyuma ulivunjika vipande kwa nguvu ya yale mawimbi. 42 Wale askari walikuwa wamepanga kuwaua wafungwa wote ili wasije wakaogelea hadi pwani na kutoroka. 43 Lakini yule Ofisa wa maas kari alitaka kumwokoa Paulo, kwa hiyo akawazuia wasitekeleze mpango wao. Akaamuru wale wanaoweza kuogelea wajitupe baharini kwanza, na waogelee kuelekea pwani; 44 na wengine wajishikize kwenye vipande vya meli waelee navyo. Kwa jinsi hii, watu wote waliokolewa wakafika nchi kavu.