2 Timotheo 1

1Kutoka kwa Paulo mtume wa Kristo Yesu kwa mapenzi ya Mungu, kulingana na ahadi ya uzima uliomo ndani ya Kristo Yesu. 2Kwa Timotheo, mwanangu mpendwa. Ninakutakia neema, rehema na amani kutoka kwa Mungu Baba na kwa Kristo Yesu Bwana wetu.

Paulo Amtia Moyo Timotheo

3Ninamshukuru Mungu ninayemtumikia kwa dhamiri safi, kama walivyomtumikia baba zangu, ninapokukumbuka usiku na mchana katika sala zangu. 4Nikiyakumbuka machozi yako, ninatamani sana kukuona ili nijazwe furaha. 5Nakumbushwa kuhusu imani yako ya kweli, imani ambayo walikuwa nayo bibi yako Loisi na mama yako Eunike na ambayo nina hakika, unayo. 6Kwa sababu hii nakukum busha ukichochee kile kipawa ulichopewa na Mungu wakati nilipo kuwekea mikono. 7Maana Mungu hakutupatia roho ya woga bali roho ya nguvu, ujasiri na kiasi.

8Basi usione haya kumshuhudia Bwana wetu, wala usinionee haya mimi niliye mfungwa kwa ajili yake, bali uishiriki taabu kwa ajili ya Habari Njema kwa kadiri ya nguvu upewayo na Mungu. 9Yeye ametuokoa na kutuita tupokee maisha ya utakatifu; si kwa sababu ya matendo yetu mema bali kwa sababu ya makusudio yake na neema yake. Tulipewa neema hii katika Kristo Yesu tangu milele 10na sasa imedhihirishwa kwa kuja kwake Mwokozi wetu Kristo Yesu ambaye ameondoa kifo kabisa na kuleta uzima na kutokufa kwa njia ya Injili. 11Nami nimechaguliwa kuwa mhubiri, mtume na mwalimu wa Injili hii. 12Ndio sababu ninateseka hivi. Lakini sioni aibu kwa maana ninamjua huyo niliyemwamini na nina hakika ya kuwa anaweza kutunza kile nilichomkabidhi, mpaka siku ile.

13Tumia kama kielelezo cha mafundisho sahihi maneno ya kweli ambayo umeyasikia kutoka kwangu pamoja na imani na upendo katika Kristo Yesu. 14Linda ile kweli ambayo umekabidhiwa na Roho Mtakatifu aishiye ndani yetu. 15Bila shaka unafahamu kuwa watu wote katika jimbo la Asia wameniacha, wakiwemo Filego na Hermogene. 16Bwana aonyeshe huruma yake kwa jamaa ya Onesiforo kwa sababu alinitia moyo mara nyingi na hakuonea aibu minyororo yangu. 17Bali alipofika Roma alinitafuta kwa bidii mpaka akanipata. 18Bwana amwezeshe kupata rehema kutoka kwa Bwana siku ile. Unafahamu pia jinsi alivyoni saidia huko Efeso.