Yohana 1

Neno Alifanyika Mwili

1Hapo mwanzo, kabla ya kuwapo kitu kingine cho chote, aliku wapo Neno. Huyo Neno alikuwa pamoja na Mungu, naye alikuwa Mungu. 2Tangu mwanzo Neno amekuwa na Mungu. 3Vitu vyote viliumbwa na yeye, wala hakuna cho chote kilichoumbwa ambacho hakukiumba. 4Uzima ulikuwa ndani yake na uzima huo ndio ulikuwa nuru ya watu. 5Nuru hiyo huangaza gizani na giza haliwezi kamwe kuizima.

6Mtu mmoja aitwaye Yohana alitumwa na Mungu 7awaambie watu kuhusu hiyo nuru, ili kwa ushuhuda wake wapate kuamini. 8Yohana mwenyewe hakuwa ile nuru. Yeye alitumwa kuishuhudia hiyo nuru. 9Nuru halisi ambayo inawaangazia watu wote ilikuwa inakuja ulim wenguni. 10Neno alikuwepo ulimwenguni, lakini japokuwa aliumba ulimwengu, watu wa ulimwengu hawakumtambua! 11Alikuja nyumbani kwake, lakini watu wake hawakumpokea! 12Bali wote waliompokea na kumwamini aliwapa haki ya kufanywa watoto wa Mungu. 13Hawa hawakuwa watoto wa Mungu kwa kuzaliwa kwa njia ya asili, wala kwa mapenzi au mipango ya watu bali wamezaliwa na Mungu mwenyewe.

14Neno akawa mwanadamu akaishi kati yetu akiwa amejaa utu kufu na kweli. Tuliona utukufu wake, utukufu wa Mwana pekee wa Baba. 15Yohana alishuhudia habari zake, akatangaza: “Huyu ndiye yule niliyewaambia kuwa, ‘Yeye ajaye baada yangu ni mkuu kuliko mimi kwa kuwa alikuwapo kabla sijazaliwa.”’ 16Na kutokana na ukamilifu wake, sisi sote tumepokea neema tele. 17Musa alitule tea sheria kutoka kwa Mungu, lakini Yesu Kristo ametuletea neema na kweli. 18Hakuna mtu aliyemwona Mungu wakati wo wote. Lakini Mwanae pekee, ambaye ana uhusiano wa karibu sana na Baba yake, amemdhihirisha Mungu kwetu.

Ujumbe Wa Yohana Mbatizaji

19Viongozi wa Wayahudi waliwatuma makuhani na Walawi wakam wulize Yohana, “Wewe ni nani?” 20Yohana akawajibu wazi wazi pasipo kuficha, “Mimi siye Kristo.” 21Wakamwuliza, “Wewe ni nani basi? Wewe ni Eliya ?” Akajibu, “Hapana, mimi siye.” “Wewe ni yule Nabii?” Akajibu, “Hapana.” 22Ndipo wakasema, “Basi tuambie wewe ni nani ili tupate jibu la kuwapelekea wale waliotutuma. Tueleze, wewe hasa ni nani?”

23Akawajibu kwa kutumia maneno ya nabii Isaya, “Mimi ni sauti ya mtu anayeita kwa sauti kuu nyikani, ‘Nyoosheni njia ata kayopita Bwana.”’ 24Baadhi ya wale waliotumwa na Mafarisayo 25walimwuliza, “Kama wewe si Kristo, wala Eliya na wala si yule Nabii, kwa nini unabatiza watu?”

26Yohana akawajibu, “Mimi ninabatiza kwa maji, lakini kati yenu yupo mtu msiyemjua. 27Yeye anakuja baada yangu, lakini mimi sistahili hata kumvua viatu vyake.”

28Mambo haya yalitokea Bethania, kijiji kilichoko ng’ambo mashariki ya mto wa Yordani, ambapo Yohana alikuwa akibatiza watu.

Mwana Kondoo Wa Mungu

29Kesho yake Yohana alimwona Yesu akimjia akasema, “Tazameni! Huyu ndiye Mwana-Kondoo wa Mungu anayeondoa dhambi ya ulimwengu! 30Huyu ndiye niliyewaambia kwamba, ‘Yeye ajaye baada yangu ni mkuu kuliko mimi kwa maana alikuwapo kabla sijazaliwa.’ 31Mimi mwenyewe sikumfahamu, lakini nimekuja nikibatiza kwa maji kusudi apate kufahamika kwa watu wa Israeli.”

32Kisha Yohana akatoa ushuhuda huu: “Nilimwona Roho akish uka kutoka mbinguni kama hua, akakaa juu yake. 33Mimi nisingem tambua, lakini Mungu ambaye alinituma nibatize watu kwa maji ali kuwa ameniambia kwamba, ‘Yule mtu utakayemwona Roho akimshukia kutoka mbinguni na kukaa juu yake, huyo ndiye atakayebatiza kwa Roho Mtakatifu.’ 34Mimi nimeona jambo hili na ninashuhudia kuwa huyu ndiye Mwana wa Mungu.”

Wanafunzi Wa Kwanza Wa Yesu

35Kesho yake, Yohana alikuwapo pale pamoja na wanafunzi wake wawili. 36Alipomwona Yesu akipita, alisema, “Tazameni! Mwana-Kondoo wa Mungu!” 37Wale wanafunzi wawili walipomsikia Yohana akisema haya, walimfuata Yesu. 38Yesu akageuka akawaona wakimfuata akawauliza, “Mnataka nini?” Wakamwambia, “Rabi’ 39Yesu akawajibu, “Njooni mkapaone!” Ilikuwa yapata saa kumi jioni. Basi wakaenda wakaona alipokuwa anaishi, wakashinda naye siku hiyo.

40Mmojawapo wa hao wanafunzi wawili waliomfuata Yesu baada ya kusikia maneno ya Yohana, alikuwa ni Andrea, ndugu yake Simoni Petro. 41Mara baada ya haya Andrea alikwenda kumtafuta ndugu yake akamwambia, “Tumemwona Masihi,” yaani Kristo. 42Andrea akampeleka Simoni kwa Yesu. Yesu akamtazama, akasema, “Wewe ni Simoni mwana wa Yohana; sasa utaitwa Kefa.” Tafsiri ya Kefa kwa Kigiriki ni Petro, maana yake ‘Mwamba’.

Yesu Anawaita Filipo Na Nathanaeli

43Kesho yake Yesu aliamua kwenda Galilaya. Akakutana na Filipo, akamwambia, “Nifuate.” 44Filipo alikuwa mwenyeji wa Bethsaida, mji ambapo Andrea na Petro walikuwa wanaishi. 45Fil ipo naye akamtafuta Nathanaeli akamwambia, “Tumekutana na Yesu wa Nazareti mwana wa Yusufu, ambaye Musa katika Torati na pia Manabii waliandika habari zake.” 46Nathanaeli akajibu, “Je, inawezekana kitu cho chote chema kikatoka Nazareti?” Filipo akamwambia, “Njoo ukajionee mwenyewe.” 47Yesu alipomwona Nathanaeli anakaribia, akasema, “Huyu ni Mwisraeli halisi. Hana udanganyifu wo wote.” 48Nathanaeli akamwuliza, “Umenifaha muje? ” Yesu akamjibu, “Nilikuona wakati ulipokuwa chini ya mtini, kabla hata Filipo hajakuita.” 49Nathanaeli akamwambia, “Mwalimu, wewe ni Mwana wa Mungu! Wewe ni Mfalme wa Israeli!” 50Yesu akamwambia, “Unaamini kwa kuwa nimekuambia kwamba nili kuona chini ya mtini? Basi utaona mambo makuu zaidi kuliko hilo!” 51Ndipo akawaambia, “Ninawaambia hakika, mtaona mbingu ikifunguka, na malaika wa Mungu wakienda mbinguni na kushuka juu yangu mimi Mwana wa Adamu.”