Yesu Anaingia Yerusalemu Kwa Shangwe
1Walipokaribia Yerusalemu, wakafika Bethfage katika mlima wa Mizeituni. Ndipo Yesu akawatuma wanafunzi wake wawili, 2 aka waagiza, “Nendeni katika kijiji kilichoko mbele yenu na mkiingia mtamwona punda amefungwa na mwanapunda pamoja naye. Wafungueni mniletee. 3 Kama mtu akiwauliza lo lote, mwambieni, ‘Bwana anawa hitaji 4 Haya yalitokea ili kutimiza utabiri wa nabii aliposema, 5 ‘Mwambieni binti Sayuni, tazama mfalme wako anakuja kwako ni mnyenyekevu, na amepanda punda, mwanapunda, mtoto wa punda.’
6 Wale wanafunzi wakaenda, wakafanya kama Yesu alivyowaagiza. 7 Wakamleta yule punda na mwanapunda. Wakatandika mavazi yao juu ya hao punda na Yesu akaketi juu yake. 8 Umati mkubwa wa watu wakatandika nguo zao barabarani, wengine wakakata matawi ya miti wakayatandaza barabarani. 9 Ule umati wa watu waliomtangulia na wale waliomfuata wakapiga kelele wakisema, “Hosana kwa Mwana wa Daudi . Amebarikiwa anayekuja kwa jina la Bwana! Hosana juu mbin guni.”
10 Yesu alipoingia Yerusalemu, mji wote ukajawa na hekaheka, watu wakauliza, “Huyu ni nani?” 11 Ule umati wa watu wakajibu, “Huyu ni Yesu, yule nabii kutoka Nazareti katika Galilaya.”
Yesu Afukuza Wafanya Biashara Hekaluni
12 Yesu aliingia katika eneo la Hekalu akawafukuza wote wali okuwa wakinunua na kuuza vitu Hekaluni. Akazipindua meza za watu waliokuwa wakibadilisha fedha na viti vya wale waliokuwa wakiuza njiwa. 13 Akawaambia, “Imeandikwa katika Maandiko, ‘Nyumba yangu itaitwa nyumba ya sala,’ lakini ninyi mmeigeuza kuwa pango la wanyang’anyi.”
14 Vipofu na vilema wakamwendea, naye akawaponya. 15 Lakini makuhani wakuu na walimu wa sheria waliudhika walipoona mambo ya ajabu aliyoyafanya na kuwasikia watoto wakishangilia Hekaluni wakisema, “Hosana kwa Mwana wa Daudi!” Wakamwuliza Yesu, 16 “Unasikia hawa wanavyosema?” Akawajibu, “Nasikia. Kwani hamjasoma maneno haya, ‘Kutoka katika vinywa vya watoto wadogo na wale wanaonyonya umeleta sifa kamili’? ” 17 Akawaacha akatoka nje ya mji, akaenda hadi Bethania, akalala huko.
18 Asubuhi, Yesu alipokuwa akirudi mjini, aliona njaa. 19 Alipoona mtini kando ya bara bara aliusogelea akakuta hauna tunda lo lote ila majani tu. Akaulaani akisema, “Usizae matunda kamwe!” Wakati huo huo ule mtini ukanyauka. 20 Wanafunzi wake wakashangazwa na tukio hilo wakamwuliza, “Imekuwaje mtini huu ukanyauka ghafla?” 21 Yesu akawajibu, “Nawaambia kweli, kama mna imani na msiwe na mashaka hata kidogo, mtaweza kufanya yaliy ofanyika kwa huu mtini; na hata mkiuambia mlima huu, ‘Ng’oka, nenda kajitupe baharini,’ itafanyika. 22 Na lo lote mtakaloomba katika sala, mtapewa, kama mna imani.”
Yesu Aulizwa Kuhusu Mamlaka Yake
23 Yesu alipoingia tena Hekaluni, makuhani wakuu na wazee walimjia alipokuwa akifundisha, wakamwuliza, “Unafanya mambo haya kwa mamlaka gani na ni nani amekupa mamlaka hayo?” 24 Yesu akawajibu, “Na mimi nitawauliza swali na mkinijibu nami nita waambia ni kwa mamlaka gani ninafanya mambo haya. 25 Ubatizo wa Yohana ulitoka wapi? Mbinguni au kwa watu?” Wakaanza kubishana kati yao wakisema, “Tukisema ulitoka mbinguni atatuuliza, ‘Mbona basi hamkumwamini?’ 26 Lakini tukisema ulitoka kwa wanadamu, tunaogopa hawa watu, maana wote wanamtambua Yohana kuwa ni nabii.” 27 Kwa hiyo wakamjibu Yesu, “Hatufahamu.” Naye aka waambia, “Nami sitawaambia ni kwa mamlaka gani ninatenda mambo haya.”
Mfano Wa Wana Wawili
28 ‘Lakini mwaonaje? Mtu mmoja alikuwa na watoto wawili wa kiume. Akamwendea yule wa kwanza akamwambia, ‘Mwanangu, nenda ukafanye kazi kwenye shamba la mizabibu leo.’ 29 Yule mwanae akasema, ‘Siendi,’ lakini baadaye akabadili mawazo akaenda. 30 Kisha yule baba akamwendea yule mwanae mwingine akamwambia vile vile. Yeye akajibu, ‘Nitakwenda baba,’ lakini asiende. 31 Ni yupi kati yao aliyetimiza alivyotaka baba yake?” Wakamjibu, “Yule wa kwanza.” Yesu akawaambia, “Nawaambieni kweli, watoza ushuru na makahaba wanawatangulia kuingia katika Ufalme wa Mungu.
32 Kwa maana Yohana alikuja kwenu kuwaonyesha njia ya haki, lakini hamkumwamini, ila watoza ushuru na makahaba walimwamini. Nanyi hata mlipoona hayo, baadaye hamkutubu na kum wamini.”
Mfano Wa Wapangaji Waovu
33 “Sikilizeni mfano mwingine: mtu mmoja mwenye shamba alilima shamba akapanda mizabibu. Akalizungushia ua, na ndani yake akachimba kisima cha kusindikia zabibu; na akajenga mnara. Kisha akalikodisha hilo shamba kwa wakulima fulani, akasafiri kwenda nchi nyingine.
34 “Wakati wa mavuno ulipokaribia aliwatuma watumishi wake kwa hao wakulima kupokea mavuno yake. 35 Wale wakulima wakawaka mata wale watumishi; wakampiga mmoja, wakamwua mwingine na kum piga mawe mwingine. 36 Akatuma watumishi wengine, wengi kuliko wale wa mwanzo. Wale wakulima wakawatendea vile vile. 37 Mwish owe akamtuma mwanae kwao akisema, ‘Bila shaka watamheshimu mwa nangu.’ 38 Lakini walipomwona mwanae, waliambiana, ‘Huyu ndiye mrithi. Njooni tumwue tuchukue urithi wake.’ 39 Basi wakamchu kua, wakamtupa nje ya shamba la mizabibu, wakamwua. 40 Sasa, akija yule mwenye shamba, mnadhani atawafanya nini hao waku lima?” 41 Wakamjibu, “Atawaangamiza kabisa hao wadhalimu na kulipangisha shamba lake kwa wakulima wengine ambao watampatia matunda yake wakati wa mavuno.”
42 Yesu akawaambia, “Hamjapata kusoma katika Maandiko kwamba: ‘Lile jiwe walilokataa wajenzi limekuwa jiwe kuu la pembeni; Bwana ndiye amefanya jambo hili nalo ni zuri ajabu machoni petu’?
43 Kwa hiyo ninawaambia, Ufalme wa Mungu utaondolewa kwenu na watapewa watu wawezao kutoa matunda yake.” [ 44 “Na ambaye ataanguka kwenye jiwe hili atavunjika vipande vipande, lakini yule litakayemwangukia atasagika sagika.”]
45 Makuhani wakuu na Mafarisayo waliposikia mifano yake, walitambua kuwa alikuwa akiwasema wao. 46 Wakatafuta njia ya kumkamata lakini waliogopa ule umati wa watu kwa kuwa wao walim tambua Yesu kuwa nabii.