Yesu Afundisha Kuhusu Talaka
1Yesu alipomaliza kusema maneno haya, aliondoka Galilaya akaenda sehemu za Yudea, ng’ambo ya mto Yordani. 2 Umati mkubwa wa watu walimfuata, naye akawaponya huko.
3 Baadhi ya Mafarisayo wakamjia wakamtega kwa kumwuliza, “Ni halali mtu kumwacha mke wake kwa sababu yo yote ile?”
4 Akawajibu, “Hamjasoma kwamba aliyewaumba tangu mwanzo ali waumba mume na mke 5 akawaambia, ‘Kwa sababu hii mtu atamwacha baba yake na mama yake na aambatane na mkewe; na hao wawili wata kuwa mwili mmoja’? 6 Kwa hiyo hawawi wawili tena, bali ni mwili mmoja. Kwa hiyo alichokiunganisha Mungu, mwanadamu asikitengan ishe.”
7 Wakamwuliza, “Kwa nini basi Musa aliagiza kwamba mtu anaweza kumpa mkewe hati ya talaka na kumwacha?” 8 Yesu akawa jibu, “Musa aliwaruhusu kuwaacha wake zenu kwa sababu mioyo yenu ni migumu. Lakini tangu mwanzo haikukusudiwa iwe hivyo. 9 Nami nawaambieni, mtu ye yote anayemwacha mkewe, isipokuwa kwa sababu ya uasherati, akaoa mke mwingine, anazini.” [“Na mtu anayemwoa mwanamke aliyepewa talaka pia anazini.”]
10 Wanafunzi wake wakamwambia, “Kama hivi ndivyo hali ilivyo kati ya mume na mke, basi ni afadhali mtu asioe!” 11 Yesu akajibu, “Si kila mtu anaweza kupokea mafundisho haya isipokuwa wale ambao Mungu amewajalia. 12 Kwa maana wako watu wasioweza kuoa kwa sababu wamezaliwa na hali hiyo; na wengine wamefanywa hali hiyo na binadamu; na pia wako wengine ambao wameamua kutokuoa kwa ajili ya Ufalme wa mbinguni. Awezaye kuli pokea fundisho hili na alipokee.”
Yesu Awabariki Watoto Wadogo
13 Kisha watoto wadogo wakaletwa kwa Yesu ili aweke mikono yake juu yao na awaombee. Lakini wanafunzi wake wakawakemea wali owaleta. 14 Yesu akawaambia, “Waacheni watoto waje kwangu, msiwazuie; kwa maana Ufalme wa mbinguni ni wa walio kama hawa. 15 Alipokwisha wawekea mikono akaondoka.
Mtu Tajiri
16 Mtu mmoja alikuja kwa Yesu akamwuliza, “Mwalimu, nifanye jambo gani jema ili nipate uzima wa milele?”
17 Yesu akamjibu, “Mbona unaniuliza kuhusu jambo jema? Kuna mmoja tu aliye mwema . Lakini kama unataka kuingia uzimani, tii amri.”
18 Yule mtu akamwuliza, “Amri zipi?” Yesu akamjibu, “Usiue, usizini, usiibe, usishuhudie uongo, 19 waheshimu baba yako na mama yako na umpende jirani yako kama nafsi yako.”
20 Yule kijana akasema, “Zote hizi nimezitii. Ninapungukiwa na nini zaidi?”
21 Yesu akamwambia, “Kama ukitaka kuwa mkamilifu, nenda kauze vitu vyote ulivyo navyo na fedha utakazopata uwape maskini, nawe utakuwa umejiwekea hazina mbinguni. Kisha njoo, unifuate.” 22 Yule kijana aliposikia hayo aliondoka kwa masikitiko, kwa sababu alikuwa tajiri sana.
Hatari Za Utajiri
23 Kisha Yesu akawaambia wanafunzi, “Nawaambieni kweli, itakuwa vigumu kwa mtu tajiri kuingia katika Ufalme wa mbinguni. 24 Tena nawaambieni, ni rahisi zaidi kwa ngamia kupita katika tundu la sindano kuliko mtu tajiri kuingia katika Ufalme wa mbinguni.” 25 Wanafunzi wake waliposikia haya walishangaa sana, wakamwuliza, “Ni nani basi anaweza kuokoka?” 26 Lakini Yesu akawatazama akawaambia, “Kwa binadamu jambo hili haliwezekani, lakini kwa Mungu kila kitu kinawezekana.” 27 Ndipo Petro aka mwambia, “Na sisi tulioacha kila kitu tukakufuata tutapata nini?”
28 Yesu akawajibu, “Ninawahakikishia kwamba, katika dunia mpya, wakati mimi Mwana wa Adamu nitakapoketi kwenye kiti changu cha utukufu cha enzi, ninyi mlionifuata pia mtaketi katika viti vya enzi kumi na viwili, mkiyahukumu yale makabila kumi na mawili ya Israeli. 29 Na kila mtu aliyeacha nyumba au ndugu zake au dada zake au baba au mama au watoto wake au mashamba kwa ajili ya jina langu, atapokea mara mia zaidi ya hayo, na atarithi uzima wa milele. 30 Lakini wengi walio wa kwanza watakuwa wa mwisho na walio wa mwisho watakuwa wa kwanza.”