Mfano Wa Mbegu
1Siku hiyo hiyo Yesu alitoka nyumbani akaketi kando ya bahari. 2 Umati mkubwa mno wa watu wakasongamana hata ikabidi aingie katika mashua akaketi humo; na wale watu wakakaa ukingoni mwa bahari. 3 Kisha akawaambia mambo mengi kwa mifano, akasema: “Mpanzi alikwenda kupanda mbegu. 4 Alipokuwa akitawanya mbegu, baadhi zikaanguka njiani, ndege wakaja wakazila. 5 Nyingine zikaanguka kwenye mawe, ambapo hapakuwa na udongo wa kutosha. Zikakua haraka kwa sababu udongo ulikuwa kidogo. 6 Lakini jua kali lilipowaka, mimea hiyo ilinyauka na kukauka kwa sababu mizizi yake haikwenda chini. 7 Mbegu nyingine zilianguka kwenye miiba. Miiba hiyo ikakua ikazisonga. 8 Mbegu nyingine zilianguka kwenye udongo mzuri zikatoa mazao, nyingine mara mia moja zaidi ya mbegu zilizopandwa, nyingine mara sitini na nyingine mara the lathini. 9 Mwenye nia ya kusikia na asikie.”
Sababu Ya Kufundisha Kwa Mifano
10 Wanafunzi wake wakamwendea wakamwuliza, “Kwa nini unazungumza na watu kwa mifano?” 11 Akawajibu, “Ninyi mmejal iwa kuzifahamu siri za Ufalme wa mbinguni, lakini wao hawakujal iwa. 12 Kwa maana mtu aliye na kitu ataongezewa mpaka awe navyo tele; lakini mtu asiye na kitu, hata kile alichonacho atany ang’anywa. 13 Hii ndio sababu nazungumza nao kwa mifano; wanata zama lakini hawaoni, wanasikiliza lakini hawasikii, wala hawae lewi. 14 Hali yao inatimiza ule utabiri wa nabii Isaya ali posema:’Hakika mtasikiliza lakini hamtaelewa, na pia mtatazama lakini hamtaona. 15 Kwa maana mioyo ya watu hawa imekuwa mizito, hawasikii kwa masikio yao, na wamefumba macho yao. Wasije wakaona kwa macho yao, na kusikia kwa masikio yao, na kuelewa kwa mioyo yao, wakanigeukia, nami nikawaponya.’ 16 Lakini macho yenu yame barikiwa, kwa maana yanaona, na masikio yenu yamebarikiwa kwa maana yanasikia. 17 Nawaambieni kweli, manabii wengi na wenye haki walitamani kuona mnayoyaona, na hawakuyaona; na kusikia mnayosikia lakini hawakuyasikia.”
Maelezo Ya Mfano Wa Mbegu
18 “Sikilizeni basi maana ya ule mfano wa mpanzi aliyepanda mbegu. 19 Mtu anaposikia neno la Ufalme na asilielewe, yule mwovu huja na kunyakua kile kilichopandwa moyoni mwake; hii ndio mbegu iliyopandwa njiani. 20 Mbegu iliyopandwa kwenye mawe ni mtu yule ambaye hulisikia neno na kulipokea mara moja kwa furaha. 21 Lakini kwa kuwa hana mizizi ndani yake, neno hilo hukaa kwa muda mfupi; na inapotokea dhiki au mateso kwa ajili ya hilo neno, yeye mara moja huanguka. 22 Mbegu iliyopandwa katika miiba ni yule mtu alisikiaye neno na mahangaiko ya maisha haya na anasa za mali hulisonga lile neno na kulifanya lisizae matunda. 23 Lakini mbegu iliyopandwa kwenye udongo mzuri ni yule mtu ambaye hulisikia neno na kulielewa. Naye hakika huzaa matunda, mara mia, au mara sitini, au mara thelathini zaidi ya mbegu iliyo pandwa.”
Mfano Wa Magugu
24 Yesu akawaambia mfano mwingine, akasema, “Ufalme wa mbi nguni unaweza kufananishwa na mtu aliyepanda mbegu nzuri katika shamba lake. 25 Lakini watu walipokuwa wamelala, adui yake aka ja akapanda magugu katikati ya ngano, akaenda zake. 26 Ngano ilipoota na kuzaa, magugu nayo yakachipua.
27 “Watumishi wa yule mwenye shamba wakamwendea, wakamwul iza, ‘Bwana, si ulipanda mbegu nzuri shambani mwako? Imekuwaje kuna magugu?’ 28 Akawajibu, ‘Adui ndiye amefanya jambo hili’. Wale watumishi wakamwuliza, ‘Sasa unataka tukayang’oe?’ 29 Lakini akasema, ‘Hapana msiyang’oe, kwa maana huenda katika kung’oa magugu mkang’oa na ngano pia. 30 Acheni ngano na magugu yakue pamoja mpaka wakati wa mavuno. Wakati huo nitawaambia wavu naji wayang’oe magugu kwanza wayafunge katika mafurushi tayari kwa kuchomwa moto, lakini wavune ngano na kuikusanya ghalani mwangu.’ ”
Mfano Wa Haradali
31 Akawaambia mfano mwingine, akasema, “Ufalme wa mbinguni unafanana na punje ndogo ya haradali ambayo mtu aliichukua akaipa nda shambani mwake. 32 Ijapokuwa mbegu hiyo ni ndogo kuliko mbegu zote, lakini inapokua, mmea wake huwa mkubwa kuliko mimea yote bustanini; nao huwa mti mkubwa ambao ndege wa angani huja na kujenga viota katika matawi yake.”
Mfano Wa Chachu
33 Akawaambia mfano mwingine: “Ufalme wa mbinguni unafanana na chachu ambayo mwanamke aliichukua akaichanganya katika vipimo vitatu vya unga mpaka wote ukaumuka.”
Sababu Ya Yesu Kutumia Mifano
34 Haya yote Yesu aliwaeleza umati wa watu kwa kutumia mifano. Na hakika hakuwaambia lo lote pasipo kutumia mfano. 35 Hii ilikuwa kutimiza utabiri wa nabii, kwamba, ‘Nitazungumza nao kwa mifano; nitatamka mambo yaliyofichika tangu kuumbwa kwa ulimwengu.’
Ufafanuzi Wa Mfano Wa Magugu
36 Kisha Yesu akaagana na huo umati wa watu, akaingia nyum bani. Wanafunzi wake wakamjia wakamwambia, “Tueleze maana ya ule mfano wa magugu shambani.”
37 Akawaambia, “Aliyepanda mbegu nzuri ni mimi Mwana wa Adamu. 38 Shamba ni ulimwengu, na mbegu nzuri ni wana wa ufalme. Magugu ni wana wa yule mwovu. 39 Yule adui aliyepanda magugu ni shetani. Mavuno ni mwisho wa ulimwengu; na wavunaji ni malaika. 40 Kama vile magugu yanavyong’olewa na kuchomwa motoni, ndivyo itakavyokuwa wakati wa mwisho wa ulimwengu. 41 Mwana wa Adamu atawatuma malaika wake wang’oe kutoka katika Ufalme wake kila kitu kinachosababisha dhambi na watenda maovu wote. 42 Nao wata watupa katika tanuru la moto ambako kutakuwa na kilio na kusaga meno. 43 Ndipo wenye haki watang’aa kama jua katika Ufalme wa Baba yao. Mwenye nia ya kusikia, na asikie.”
Mfano Wa Hazina Iliyofichwa
44 “Ufalme wa mbinguni unafanana na hazina iliyofichwa shambani ambayo mtu mmoja aliigundua akaificha tena. Kisha katika furaha yake, akaenda akauza vyote alivyokuwa navyo, akanu nua lile shamba.” 45 Tena, Ufalme wa mbinguni unafanana na mfanya biashara aliyekuwa akitafuta lulu safi, 46 ambaye alipo pata lulu moja ya thamani kubwa, alikwenda akauza vyote alivyo kuwa navyo akainunua.”
Mfano Wa Wavu
47 “Na tena Ufalme wa mbinguni ni kama wavu wa kuvulia samaki ambao ulitandazwa baharini ukakamata samaki wa kila aina. 48 Ulipojaa, wavuvi waliuvuta ukingoni, wakachagua samaki wazuri wakawaweka kwenye vyombo safi, lakini wale samaki wabaya wakawat upa.
49 “Hivi ndivyo itakavyokuwa wakati wa mwisho wa dunia. Malaika watakuja na kuwatenganisha watu waovu na watu wenye haki. 50 Na watawatupa hao waovu katika tanuru ya moto ambako kutakuwa na kilio na kusaga meno. 51 Je, mmeyaelewa haya yote?” Wakam jibu, “Ndio.” 52 Akawaambia, “Basi kila mwalimu wa sheria aliye mwanafunzi wa Ufalme wa mbinguni ni kama mwenye nyumba anayetoa kutoka katika ghala yake mali mpya na mali ya zamani.”
Yesu Akataliwa Nazareti
53 Yesu alipomaliza kutoa mifano hii, aliondoka. 54 Alipo fika mji wa kwao, aliwafundisha watu katika sinagogi lao. Nao wakastaajabu, wakauliza, “Mtu huyu amepata wapi hekima hii na uwezo huu wa kufanya miujiza? 55 Huyu si yule mwana wa seremala? Mama yake si anaitwa Mariamu, na ndugu zake ni Yakobo, Yusufu, Simoni na Yuda? 56 Na dada zake si wako hapa nasi? Amepata wapi basi mambo haya yote?” 57 Wakakataa kumpokea. Lakini Yesu aka waambia, “Nabii hakosi heshima isipokuwa katika nchi yake na nyumbani kwake.”
58 Na hakufanya miujiza mingi huko kwa sababu ya kutokuamini kwao.