Ibada Ya Kiroho
1Kwa hiyo ndugu zangu nawasihi kwa sababu ya huruma zake Mungu, jitoeni kwake muwe sadaka hai, takatifu na inayompendeza Mungu, ambayo ndio ibada yenu ya kiroho. 2 Msiige tabia na mien endo ya dunia hii bali mbadilishwe, nia zenu zikifanywa kuwa mpya, ili mpate kuwa na hakika ni nini mapenzi ya Mungu: yaliyo mema, yanayopendeza machoni pake na makamilifu.
3 Kwa sababu ya neema niliyopewa nawaambia kila mmoja wenu: Msijifikirie kuwa watu wa juu kuliko mlivyo. Badala yake, muwe na kiasi katika mawazo yenu, kila mmoja wenu ajipime kutokana na kiasi cha imani aliyopewa na Mungu. 4 Kama vile ambavyo kila mmoja wenu ana mwili mmoja wenye viungo vingi, na kila kiungo kina kazi yake, 5 hali kadhalika, ndani ya Kristo sisi tulio wengi tunakuwa mwili mmoja na kila mmoja wetu ni sehemu ya we ngine wote. 6 Tumepewa vipawa tofauti kulingana na neema tuliy opokea kutoka kwa Mungu. Kama mtu ana kipawa cha kutoa unabii basi akitumie kulingana na imani yake. 7 Kama kipawa chake ni kuwahudumia wengine, basi awahudumie. Kama ni kufundisha, basi na afundishe. 8 Kama kipawa chake ni kuwatia moyo wengine, na afanye hivyo. Kama ni ukarimu, basi na atoe kwa moyo. Mwenye kipawa cha uongozi na afanye hivyo kwa bidii. Mwenye kipawa cha huruma na aonyeshe huruma yake kwa furaha.
Upendo Wa Kweli
9 Upendo wenu uwe wa kweli. Chukieni uovu, mshikilie yaliyo mema. 10 Pendaneni ninyi kwa ninyi kwa upendo wa kindugu. Waheshimuni wengine kuliko mnavyojiheshimu wenyewe. 11 Juhudi yenu isipungue, moto wenu wa kiroho uendelee kuwaka mkimtumikia Mungu. 12 Muwe na furaha katika tumaini lenu, na katika dhiki muwe na subira. Ombeni wakati wote. 13 Wasaidieni watu wa Mungu walio na shida. Muwe wakarimu kwa matendo.
14 Waombeeni baraka za Mungu wanaowatesa. Wabarikini wala msiwalaani. 15 Furahini pamoja na wenye furaha; huzunikeni pamoja na wenye huzuni. 16 Muishi kwa amani ninyi kwa ninyi. Msitake makuu bali muwe tayari kushirikiana na wanyonge. Kamwe msiwe watu wenye majivuno.
17 Msimlipe mtu uovu kwa uovu. Jitahidini kutenda yaliyo mema machoni pa watu wote. 18 Kama ikiwezekana, kaeni kwa amani na watu wote. 19 Wapendwa, msijilipizie kisasi, bali mtoe nafasi kwa ghadhabu ya Mungu, maana imeandikwa:“Kisasi ni juu yangu; Mimi nitalipa, asema Bwana. 20 Badala yake, adui yakoakiwa na njaa, mpe chakula; akiwa na kiu, mpe kitu anywe. Maana ukifanya hivyo, utampalia mkaa wa moto kichwani pake. 21 Usishindwe na ubaya, bali uushinde ubaya kwa wema.