Kuwa Na Amani Na Mungu
1Basi, kwa kuwa tumekwisha kuhesabiwa haki kwa imani, tuna amani na Mungu kwa ajili ya Bwana wetu Yesu Kristo. 2 Kwa kupitia kwake tumepata njia ya kufikia neema hii ambayo inatuwezesha kusimama imara, tukifurahia tumaini letu la kushiriki utukufu wa Mungu. 3 Zaidi ya hayo, pia tunafurahia mateso yetu kwa sababu tunafahamu kuwa mateso huleta subira; 4 na subira huleta uthabiti wa moyo; na uthabiti wa moyo hujenga tumaini. 5 Tukiwa na tumaini hatuwezi kukata tamaa kwa sababu Mungu amekwisha kumimina upendo wake mioyoni mwetu kwa njia ya Roho Mtakatifu ambaye ni zawadi tuliyopewa na Mungu.
6 Tulipokuwa tungali wanyonge, wakati aliochagua Mungu, Kristo aliwafia wenye dhambi. 7 Ni vigumu sana kwa mtu kujitolea kufa kwa ajili ya mwenye haki, ingawa yawezekana mtu akajitolea kufa kwa ajili ya mtu mwema. 8 Lakini Mungu anaudhihirisha upendo wake kwetu kwamba: tulipokuwa tungali wenye dhambi, Kristo ali kufa kwa ajili yetu.
9 Basi, kwa kuwa tumekwisha kuhesabiwa haki kwa damu yake, bila shaka atatuokoa kutoka katika ghadhabu ya Mungu. 10 Kwa kuwa kama tulipokuwa maadui wa Mungu tulipatanishwa kwa kifo cha Mwanae, bila shaka sasa kwa kuwa tumepatanishwa, tutaokolewa kwa uzima wake. 11 Si hivyo tu, bali pia tunamfurahia Mungu katika Bwana wetu Yesu Kristo ambaye kwa ajili yake tumepokea upatanisho wetu.
Adamu Alileta Kifo, Yesu Ameleta Uzima
12 Kwa hiyo kama vile ambavyo dhambi iliingia ulimwenguni kupitia kwa mtu mmoja, na dhambi ikaleta kifo, na kwa njia hiyo kifo kikawajia watu wote kwa kuwa wote walitenda dhambi -
13 kwa maana kabla sheria haijatolewa dhambi ilikuwepo ulimwenguni. Lakini dhambi haihesabiwi ambapo hakuna sheria. 14 Hata hivyo tangu wakati wa Adamu hadi wakati wa Musa, kifo kiliwatawala watuwote hata wale ambao dhambi zao hazikuwa kama uasi wa Adamu. Adamu alikuwa mfano wa yule ambaye angalikuja. 15 Lakini zawadi iliyotolewa bure haiwezi kulinganishwa na ule uasi. Kwa maana ikiwa watu wengi walikufa kwa sababu ya uasi wa mtu mmoja, basi neema ya Mungu na zawadi iliyotolewa kwa ajili ya mtu mmoja, Yesu Kristo, imemiminika kwa wingi zaidi kwa watu wengi. 16 Pia zawadi ya Mungu sio kama matukio ya ile dhambi ya mtu mmoja. Kwa maana hukumu iliyotokana na uasi huo ilileta laana, lakini zawadi iliyopatikana bure baada ya dhambi nyingi, inaleta haki ya Mungu. 17 Na ikiwa kutokana na uasi wa mtu mmoja kifo kilitawala kupitia huyo mtu mmoja, wale wanaopokea wingi wa neema na zawadi ya bure ya kuhesabiwa haki, watatawala zaidi sana katika maisha kwa ajili ya huyo mtu mmoja, Yesu Kristo. 18 Kwa hiyo, kama vile uasi wa mtu mmoja ulivyoleta hukumu kwa watu wote, hali kadhalika, tendo la haki la mtu mmoja linawafanya watu wote waachiliwe huru na kupewa uzima. 19 Na kama vile ambavyo watu wengi walifanywa kuwa wenye dhambi kwa ajili ya kutokutii kwa mtu mmoja, vivyo hivyo wengi watahesabiwa haki na Mungu kwa ajili ya utii wa mtu mmoja.
20 Sheria ililetwa ili dhambi iongezeke. Lakini dhambi ili poongezeka, neema iliongezeka zaidi. 21 Kama vile ambavyo dhambi ilitawala kwa njia ya kifo, vivyo hivyo neema ya Mungu iweze kutawala kwa njia ya haki, ikileta uzima wa milele katika Yesu