Kutii Mamlaka
1Kila mtu hana budi kutii serikali inayotawala. Kwa maana hakuna mamlaka isiyotoka kwa Mungu; na serikali zote zilizopo zimewekwa na Mungu. 2Kwa hiyo anayepinga mamlaka inayotawala ana pinga chombo kilichowekwa na Mungu; na watu wanaoasi watajiletea hukumu. 3Kwa maana watawala hawatishi watu wanaotenda mema bali wale wanaotenda maovu. Kama hupendi kuishi kwa kumwogopa mwenye mamlaka, basi tenda mema naye atakusifu. 4Maana mwenye mamlaka ni mtumishi wa Mungu kwa manufaa yako. Lakini kama ukitenda maovu, basi ogopa kwa maana hatembei na silaha bure. Yeye ni mtumishi wa Mungu anayetekeleza adhabu ya Mungu juu ya watenda maovu. 5Kwa hiyo ni lazima kutii wenye mamlaka, si kwa sababu ya kuogopa adhabu tu bali pia kwa ajili ya dhamiri.
6Kwa sababu hiyo hiyo mnalipa kodi, kwa maana watawala ni watumishi wa Mungu ambao hutumia muda wao wote kutawala. 7Wal ipeni wote haki zao; mtu wakodi mlipe kodi; na mtoza ushuru mli pe ushuru; astahilie kunyenyekewa, mnyenyekee; astahiliye hesh ima, mheshimu.
Upendo Na Sheria
8Msiwe na deni la mtu ye yote; isipokuwa deni la kupendana; kwa maana ampendaye mwenzake, ameitimiza sheria. 9Kwa maana amri zisemazo: Usizini, Usiue, Usiibe, Usitamani na amri nyingine zote, zinajumlishwa katika amri hii moja: “Mpende jirani yako kama nafsi yako.” 10Upendo haumfanyii jirani jambo baya, kwa hiyo upendo unakamilisha sheria zote.
11Fanyeni hivi mkitambua kuwa sasa tumo katika wakati gani. Huu ni wakati wa kuamka kutoka usingizini, kwa maana wokovu wetu umekaribia zaidi sasa kuliko wakati tulipoamini kwa mara ya kwanza. 12Usiku unakwisha na mchana unakaribia. Kwa hiyo tutupe kando matendo ya giza, tuvae silaha za nuru. 13Tuishi maisha ya heshima kama inavyopasa wakati wamchana: si kwa ulafi na ulevi; si kwa ufisadi na uasherati; si kwa ugomvi na wivu. 14Bali jivikeni Bwana Yesu Kristo, na msitoe nafasi kwa miili yenu yenye asili ya dhambi, kutimiza tamaa zake.