Ufunua wa Yohana 4

Kiti Cha Enzi Kilichoko Mbinguni

1Baada ya hayo nilitazama, nikaona mlango ulio wazi mbin guni. Na ile sauti niliyokuwa nimeisikia ikisema nami kama tar umbeta ikasema, “Njoo huku juu nami nitakuonyesha yatakayotokea baada ya haya. ” Ghafla nilikuwa katika Roho, na mbele yangu kilikuwapo kiti cha enzi mbinguni, kikiwa kimekaliwa. Aliyeketi kwenye kiti hicho cha enzi alionekana kama jiwe zuri jekundu na akiki, na upinde wa mvua ulizunguka kile kiti cha enzi, ukione kana kama zumaridi. Kiti hicho kilizungukwa na viti vingine ishirini na vinne vya enzi ambavyo juu yake walikaa wazee ishi rini na wanne waliokuwa wamevalia mavazi meupe na taji za dhahabu vichwani. Na katika kile kiti cha enzi kulitoka umeme, ngurumo na sauti. Taa saba za moto zilikuwa zinawaka mbele ya kile kiti cha enzi, ambazo ni zile roho saba za Mungu. Mbele ya kile kiti cha enzi kulikuwa na kitu kinachofanana na bahari ya kioo iking’aa kama jiwe la kioo. Katikati, kuzunguka kile kiti cha enzi, walikuwapo viumbe hai wanne, wenye macho kila mahali, mbele na nyuma.

Kiumbe hai wa kwanza alifanana na simba, wa pili alifanana na ng’ombe dume, wa tatu alikuwa na uso kama wa mwanadamu, wa nne alifanana na tai arukaye. Na hawa viumbe hai wanne, kila mmoja alikuwa na mabawa sita na macho kila mahali, hata chini ya mabawa. Usiku na mchana hawakuacha kuimba, “Mtakatifu, Mtakatifu, Mtakatifu, ni Bwana Mungu Mwenyezi, aliyekuwako, aliyeko na atakayekuja.”

Kila mara viumbe hao wanne walipomtukuza na kumheshimu na kumshukuru yeye aliyeketi kwenye kiti cha enzi na aishie milele na milele, 10 wale wazee ishirini na wanne walianguka mbele zake yeye aliyeketi kwenye kiti cha enzi na kumwabudu yeye aliye hai milele na milele. Wakaziweka taji zao mbele ya kile kiti cha enzi wakisema, 11 “Bwana wetu na Mungu wetu, wewe umestahili kupokea utukufu na heshima na uweza, kwa maana ni wewe uliyeviumba vitu vyote, na kwa mapenzi yako vitu vyote viliumbwa na vinapata kuwapo.”