Ufunua wa Yohana 14

Mwana-Kondoo Na Waliokombolewa Wa Kwanza

1Kisha nikatazama na mbele yangu nikamwona Mwana-Kondoo amesimama juu ya Mlima Sioni akiwa pamoja na watu 144,000 ambao kwenye vipaji vya nyuso zao waliandikwa jina la Mwana-Kondoo na jina la Baba yake. Basi nikasikia sauti kutoka mbinguni kama sauti ya maporomoko ya maji mengi na kama sauti ya ngurumo ya radi kubwa. Na sauti hiyo niliyoisikia, ilikuwa kama sauti ya wapiga vinubi wakipiga vinubi vyao. Walikuwa wanaimba wimbo mpya mbele ya kiti cha enzi na mbele ya wale viumbe hai wanne na wale wazee. Hakuna mtu aliyeweza kujifunza wimbo huo isipokuwa hao watu 144,000 waliokombolewa kutoka duniani. Hao ndio wale ambao hawakujitia unajisi kwa kuhusiana na wanawake, kwa kuwa wao ni bikira. Hao ndio wanaomfuata Mwana-Kondoo kila aendako. Wame nunuliwa kutoka miongoni mwa wanadamu wakawa matunda ya kwanza kutolewa kwa Mungu na kwa Mwana-Kondoo. Hawajapata kusema uongo kamwe; hawana hatia yo yote.

Malaika Watatu

Kisha nikamwona malaika mwingine akiruka juu angani akiwa na Injili ya milele ya kuwatangazia watu wote waishio duniani: kwa mataifa yote, makabila yote, kwa watu wa lugha zote na watu wa aina zote. Akasema kwa sauti kuu, “Mcheni Mungu na kumtu kuza kwa maana saa ya kutoa hukumu yake imefika. Mwabuduni yeye aliyeumba mbingu, dunia, bahari na chemchemi za maji.”

Malaika wa pili akafuata akisema, “Babiloni umeanguka! Babiloni mkuu umeanguka, ule mji mkuu ambao uliwanywesha mataifa yote divai yake, divai kali ya uzinzi wake.”

Malaika wa tatu aliwafuata hao wawili akisema kwa sauti kuu, “Kama mtu ye yote anamwabudu yule mnyama na sanamu yake na kukubali kutiwa alama yake kwenye kipaji cha uso wake au kwenye mkono wake, 10 yeye naye atakunywa divai ya ghadhabu ya Mungu ambayo imemiminiwa katika kikombe cha ghadhabu yake bila kuchan ganywa na maji. Naye atateswa kwa moto na kiberiti mbele ya mal aika watakatifu na mbele za Mwana-Kondoo. 11 Moshi wa mateso yao hupanda juu milele na milele; wala hakuna nafuu, mchana au usiku, kwa wale wamwabuduo huyo mnyama na sanamu yake au kwa ye yote anayepokea alama ya jina lake.” 12 Jambo hili linahitaji watu wa Mungu, wale ambao wanazishika amri zake, wawe wavumilivu na kumwamini Yesu.

13 Kisha nikasikia sauti kutoka mbinguni ikisema, “Andika haya: Wamebarikiwa watu ambao tangu sasa wanakufa wakiwa ndani ya Bwana.” “Naam,” asema Roho, “watapumzika baada ya taabu zao, kwa kuwa matendo yao yatawafuata.”

Mavuno

14 Nikatazama, na mbele yangu nikaona wingu jeupe na mtu anayeonekana kama ‘mwana wa mtu’ akiwa ameketi juu yake. Alikuwa na taji ya dhahabu kichwani mwake na mundu mkali mkononi mwake. 15 Na malaika mwingine akaja kutoka Hekaluni na kwa sauti kubwa akamwita yule aliyekuwa ameketi juu ya wingu akasema, “Chukua mundu wako ukavune kwa kuwa saa ya kuvuna imefika, maana mavuno ya dunia yamekomaa.” 16 Basi yule aliyekuwa amekaa juu ya wingu akauzungusha mundu wake duniani, na mavuno ya dunia yakavunwa.

17 Kisha malaika mwingine akatoka Hekaluni mbinguni, naye pia akiwa na mundu mkali.

18 Na malaika mwingine, ambaye alikuwa na mamlaka juu ya moto, akatoka kwenye madhabahu akamwita yule malaika mwenye mundu mkali kwa sauti kuu, akasema, “Chukua mundu wako mkali ukayakate matawi ya mizabibu ya dunia, maana zabibu zake zimeiva.”

19 Basi malaika huyo akauzungusha mundu wake duniani akakata zabibu za dunia, akazitia ndani ya mtambo mkubwa wa kusindika zabibu wa ghadhabu ya Mungu. 20 Zabibu zikakamuliwa ndani ya mtambo huo wa kusindika zabibu uliokuwa nje ya mji, na damu ika tiririka kama mafuriko kutoka katika mtambo huo na urefu wa mafu riko hayo ulikuwa kama kilometa mia tatu, na kina chake kiasi cha meta moja na nusu.