Yerusalemu Mpya
1Kisha nikaona mbingu mpya na dunia mpya; maana mbingu ya kwanza na dunia ya kwanza zilikwisha kutoweka na bahari haikuwapo tena. 2 Ndipo nikaona mji mtakatifu, Yerusalemu mpya, ukishuka kutoka mbinguni kwa Mungu, ukiwa umeandaliwa kama bibi harusi aliyepambwa kwa bwana wake. 3 Nikasikia sauti kubwa kutoka katika kile kiti cha enzi ikisema, “Tazama, maskani ya Mungu yako pamoja na wanadamu, naye ataishi pamoja nao. Watakuwa watu wake, na Mungu mwenyewe atakuwa pamoja nao, naye atakuwa Mungu wao. 4 Atafuta machozi yao yote, na kifo hakitakuwepo tena, wala maom bolezo, wala kilio, wala maumivu; maana mambo hayo yote ya awali yamekwisha toweka.”
5 Na yule aliyeketi juu ya kile kiti cha enzi akasema, “Tazama, nafanya kila kitu kuwa kipya.” Pia akasema, “Andika haya, maana maneno haya ni ya kuaminika, tena ni ya kweli.” 6 Akaniambia, “Yamekamilika! Mimi ni Alfa na Omega, mwanzo na mwisho. Walio na kiu nitawapa maji kutoka katika chemchemi ya maji ya uzima bila malipo. 7 Atakayeshinda atarithi baraka zote hizi, na mimi nitakuwa Mungu wake, naye atakuwa mwanangu. 8 Lakini waoga, na wasioamini na wachafu, na wauaji, na wazinzi, na wachawi, na wanaoabudu sanamu, pamoja na waongo wote, urithi wao upo katika lile ziwa linalowaka moto na kiberiti. Hii ndio mauti ya pili.”
9 Kisha mmoja wa wale malaika saba waliokuwa na mabakuli saba ya yale maafa saba ya mwisho akaja akaniambia, “Njoo, nitakuon yesha bibi harusi, mke wa Mwana-Kondoo.”
10 Basi, nikiwa katika Roho, akanipeleka mbali kwenye mlima mkubwa na mrefu, akanionyesha ule mji mtakatifu, Yerusalemu, ukishuka kutoka mbinguni kwa Mungu. 11 Ulikuwa na utukufu wa Mungu, uking’aa kama kito cha thamani sana, kama yaspa, na safi kama kioo. 12 Ulikuwa na ukuta mkubwa mrefu wenye milango kumi na mbili na malaika kumi na wawili milangoni. Kwenye milango hiyo yaliandikwa majina ya yale makabila kumi na mawili ya Israeli . 13 Ilikuwapo milango mitatu mashariki, mitatu kaskazini, mitatu kusini na mitatu magharibi. 14 Ukuta wa mji huo ulikuwa na mis ingi kumi na mbili na juu yake yaliandikwa majina ya wale mitume kumi na wawili wa Mwana-Kondoo.
15 Huyo malaika aliyesema nami alikuwa na kipimo cha dhahabu cha kupimia huo mji na milango yake na kuta zake.
16 Mji huo ulikuwa wa mraba, marefu yake yakilingana na mapana yake. Akaupima mji huo kwa hicho kipimo chake; ulikuwa kama kilometa elfu mbili na mia nne kwa upana wake, na urefu wake pamoja na kina chake vilikuwa sawa. 17 Kisha akapima na ukuta wake, urefu wake ulikuwa zaidi ya meta sitini kwa kipimo cha binadamu alichokuwa akitumia huyo malaika. 18 Ukuta huo uli jengwa kwa yaspa na mji wenyewe ulijengwa kwa dhahabu safi iking’aa kama kioo. 19 Misingi ya mji huo ilipambwa kwa kila aina ya kito cha thamani. Msingi wa kwanza ulikuwa wa yaspa; wa pili yakuti samawi; wa tatu kalkedoni; wa nne zumaridi; 20 wa tano sardoniki; wa sita akiki; wa saba krisolitho; wa nane zabar ajadi; wa tisa yakuti ya njano; wa kumi krisopraso; wa kumi na moja hiakintho; wa kumi na mbili amethisto. 21 Na ile milango kumi na mbili ilikuwa ni lulu kumi na mbili, kila mlango uli tengenezwa kwa lulu moja! Barabara za mji huo zilikuwa za dhahabu safi ing’aayo kama kioo.
22 Sikuona Hekalu yo yote ndani ya mji huo kwa sababu Bwana Mungu Mwenyezi na Mwana-Kondoo ndio Hekalu la mji. 23 Mji huo hauhitaji jua wala mwezi kuangaza juu yake kwa sababu utukufu wa Mungu ndio nuru yake na Mwana-Kondoo ndiye taa yake. 24 Mataifa yote yatatembea yakiangaziwa kwa nuru yake na wafalme wa duniani wataleta utukufu wao ndani yake. 25 Milango yake itakuwa wazi mchana daima, maana hakutakuwa na usiku huko. 26 Utukufu na heshima za mataifa zitaletwa humo. 27 Lakini hakuna kitu kichafu kitakachoingia humo wala mtu ye yote atendaye mambo ya aibu au ya udanganyifu. Bali wataingia humo wale tu ambao majina yao yamean dikwa katika kitabu cha uzima cha Mwana-Kondoo.