1Basi, maadamu ahadi ya Mungu ya kuingia katika pumziko lake bado ipo, tujihadhari asije mmoja wenu akakutwa ameshindwa kuin gia huko. 2 Maana sisi tumehubiriwa Habari Njema kama vile wao walivyohubiriwa. Lakini ujumbe waliosikia haukuwasaidia kwa sababu hawakuupokea kwa imani. 3 Kwa kuwa sisi tulioamini tunain gia katika pumziko hilo, kama Mungu alivyosema, “Na katika hasira yangu nikaapa, ‘Hawataingia kwenye pumziko langu kamwe.’ Mungu alisema hivyo ingawa kazi yake ilikamilika tangu ulimwengu ulipoumbwa. 4 Maana mahali fulani akizungumza kuhusu siku ya saba, alisema: “Mungu alipumzika siku ya saba baada ya kazi zake zote.” 5 Na tena mahali hapo alisema: “Hawataingia kwenye pum ziko langu kamwe.” 6 Basi kwa kuwa wapo watakaoingia kwenye pum ziko hilo, na wale ambao walihubiriwa Habari Njema hapo mwanzo lakini wakashindwa kuingia kwa sababu ya kutokutii kwao, 7 kwa hiyo Mungu aliweka tena siku nyingine akaiita “Leo”; akasema kwa maneno ya Daudi miaka mingi baadaye, kama yalivyokwisha kukaririwa: “Leo mkiisikia sauti yake, msiifanye mioyo yenu kuwa migumu.”
8 Maana, kama Yoshua angalikuwa amekwisha kuwapatia pumziko, Mungu asingalizungumzia baadaye kuhusu siku nyingine. 9 Kwa hiyo basi ipo bado sabato ya mapumziko waliyowekewa watu wa Mungu; 10 kwa maana, mtu anayeingia katika pumziko la Mungu, pia hupum zika kutoka katika kazi zake kama vile Mungu alivyopumzika baada ya kazi zake.
11 Basi tujitahidi kuingia kwenye pumziko hilo asije mtu akaanguka kwa kutokuamini kama hao. 12 Kwa maana neno la Mungu ni hai tena lina nguvu; ni kali kuliko upanga wenye makali kuwili, linachoma kabisa na kutenganisha nafsi na roho, viungo vya mwili na mafuta yaliyomo ndani yake; na kutambua nia na mawazo ya mioyo ya watu. 13 Hakuna kiumbe cho chote kilichofi chika machoni pa Mungu. Kila kitu kimefunuliwa na kuwekwa wazi machoni pake yeye ambaye hatuna budi kueleza habari zetu zote kwake.
Kuhani Mkuu Yesu Kristo
14 Hivyo basi, kwa kuwa tunaye kuhani mkuu aliyepitia mbingu, Yesu Mwana wa Mungu, tushikilie kwa uthabiti imani yetu tunayoikiri. 15 Kwa maana huyu kuhani wetu mkuu si kuhani ambaye hawezi kutuhurumia katika udhaifu wetu, bali ni kuhani ambaye kwa kila hali amejaribiwa kama sisi, lakini pasipo kutenda dhambi. 16 Kwa hiyo basi, tusogelee kiti cha neema kwa ujasiri, ili tupokee rehema na kupata neema ya kutusaidia wakati wa shida.