Waebrania 8

Kuhani Mkuu Wa Agano Jipya

1Basi, katika hayo yote, tunalosema ni hili: tunaye huyo kuhani mkuu, ambaye ameketi upande wa kuume wa kiti cha Mwenyezi mbinguni. Yeye ni mhudumu wa patakatifu katika ile hema ya kweli iliyowekwa na Bwana, na wala si na wanadamu.

Kila kuhani huteuliwa ili atoe sadaka na dhabihu, kwa hiyo ilikuwa muhimu kwamba huyu kuhani naye awe na kitu cha kutoa. Kama angalikuwa duniani asingalikuwa kuhani kwa sababu wapo makuhani wanaotoa sadaka kwa mujibu wa sheria ya Mose. Wanahu dumu katika patakatifu iliyo mfano na kivuli cha ile iliyoko mbinguni. Ndio maana Mose alipokaribia kujenga ile hema takatifu aliamriwa na Mungu, akisema, “Hakikisha kuwa unafanya kila kitu kulingana na mfano ulioonyeshwa mlimani.” Lakini Yesu amepewa huduma iliyo bora zaidi kuliko yao, kama vile lile agano ambalo yeye ni mpatanishi wake, lilivyo bora zaidi kuliko lile la zamani. Agano hili jipya limejengwa juu ya ahadi bora zaidi.

Kama lile agano la kwanza lisingekuwa na upungufu, kusinge kuwapo na haja ya kuwa na agano jingine. Lakini Mungu hakurid hika na watu wake, akasema, “Siku zinakuja, asema Bwana, nitaka pofanya agano jipya na nyumba ya Israeli na nyumba ya Yuda. Agano hili halitakuwa kama lile nililofanya na baba zao siku ile nilipowashika mkono niwaongoze kutoka nchi ya Misri; kwa kuwa hawakuwa waaminifu kwa agano langu, nami nikawaacha, asema Bwana. 10 Hili ndilo agano nitakalofanya na nyumba ya Israeli siku zile zitakapowadia, asema Bwana: nitaweka sheria zangu akilini mwao, na kuziandika mioyoni mwao, nami nitakuwa Mungu wao, nao watakuwa watu wangu. 11 Haitakuwapo haja tena kwao kumfundisha kila mtu mwenzake, au kila mtu ndugu yake, na kusema, ‘Mfahamu Bwana,’ kwa maana wote watanifahamu, tangu aliye mdogo kabisa hadi mkubwa kuliko wote. 12 Nitawasamehe maovu yao, na dhambi zao sitazikum buka tena”.

13 Anapozungumza juu ya agano jipya Mungu anahesabu lile agano la kwanza kuwa limechakaa, na kitu kilichochakaa na kuzeeka kitatoweka baada ya muda mfupi.