Yesu Amponya Mtu Mwenye Pepo
1Wakafika upande wa pili wa ziwa wakaingia katika jimbo la Wagerasi. 2Yesu alipotoka kwenye mashua, mtu mmoja mwenye pepo mchafu alitoka makaburini akaja kukutana naye. 3Mtu huyu aliishi makaburini wala hakuna aliyeweza kumfunga hata kwa minyororo , 4kwa maana mara nyingi alipofungwa kwa minyororo mikononi na vyuma miguuni, aliivunjavunja na hakuna mtu aliyekuwa na nguvu za kumshinda. 5Usiku na mchana alikaa makaburini na milimani aki piga makelele na kujikatakata kwa mawe.
6Alipomwona Yesu kwa mbali, alimkimbilia akapiga magoti mbele yake, 7akapiga kelele kwa nguvu akasema, “Unataka nini kwangu, Yesu, Mwana wa Mungu Mkuu? Ninakusihi kwa jina la Mungu, usinitese!” 8Alisema hivi kwa kuwa Yesu alikuwa akimwambia, “Mtoke huyu mtu! Wewe pepo mchafu!”
9Yesu akamwuliza, “Jina lako ni nani?” Akamjibu, “Jina langu ni jeshi, kwa maana tupo wengi.” 10Akamwomba sana Yesu asiwapeleke nje ya jimbo lile. 11Hapo hapo lilikuwapo kundi la nguruwe likilisha kando ya mlima. 12Wale pepo wakamsihi Yesu, “Turuhusu tukawaingie wale nguruwe.” 13Basi akawaruhusu. Wakamtoka yule mtu wakaenda wakawaingia wale nguruwe na kundi lote la nguruwe wapatao elfu mbili likatimka kasi kwenye mteremko ule, wakazama ziwani, wakafa.
14Wale waliokuwa wakichunga hao nguruwe wakakimbilia mjini na vijijini kueleza yaliyotokea. Watu wakatoka kwenda kujionea mambo hayo.
15Wakaja kwa Yesu, wakamwona yule mtu aliyekuwa amepagawa na pepo akiwa ameketi, amevaa nguo na pia akiwa na akili timamu. Wakaogopa. 16Wale walioyaona mambo haya waliwaeleza wengine yaliyomto kea yule aliyekuwa na pepo na lile kundi la nguruwe. 17Basi watu wakaanza kumwomba Yesu aondoke katika wilaya yao.
18Yesu alipoanza kuingia kwenye mashua, yule mtu aliyekuwa amepagawa na pepo akamsihi Yesu waende pamoja. 19Yesu akamka talia. Badala yake akamwambia, “Nenda nyumbani kwa jamaa yako ukawaeleze mambo makuu aliyokutendea Bwana na jinsi alivyokuhuru mia.” 20Yule mtu akaenda akaanza kutangaza katika Dekapoli - yaani miji kumi, mambo makuu aliyomtendea Bwana. Na watu wote wakastaajabu.
Yesu Amponya Mama Aliyetokwa Damu
21Yesu alipokwisha vuka tena na kufika ng’ambo ya pili, umati mkubwa wa watu ukamzunguka, yeye akiwa kando ya ziwa. 22Kisha kiongozi mmoja wa sinagogi aliyeitwa Yairo akamjia Yesu akapiga magoti miguuni pake, 23akamsihi, “Binti yangu mdogo ni mgonjwa mahututi. Tafadhali njoo umguse kwa mikono yako apate kupona na kuishi.” 24Basi Yesu akaongozana naye. Umati mkubwa wa watu waliomfuata wakawa wanamsonga.
25Na alikuwepo mama mmoja aliyekuwa amesumbuliwa na tatizo la kutokwa damu kwa miaka kumi na miwili. 26Mama huyu alikuwa amehangaika sana, akiwa ametibiwa na waganga wa kila aina na kutumia fedha yake yote kwa waganga lakini hakupata nafuu. Hali yake ilizidi kuwa mbaya. 27Alikuwa amesikia habari za Yesu kwa hiyo alimfuata kwa nyuma, akapenyeza kati ya watu, akaligusa vazi lake. 28Maana alisema moyoni mwake, “Nikiligusa vazi lake tu, nitapona.” 29Mara damu iliyokuwa inamtoka ikakauka; akajisikia amepona kabisa.
30Yesu akafahamu kuwa nguvu zimemtoka. Akageuka, akawauliza wale watu, “Ni nani amenigusa?”
31Wanafunzi wake wakamjibu, “Mbona unauliza ni nani ameku gusa? Huoni umati huu ulivyokusonga?” 32Lakini Yesu alizidi kutazama aone ni nani aliyemgusa. 33Kisha yule mwanamke, akijua kilichomtokea, akaja, akaanguka miguuni kwake akitetemeka kwa hofu, akamweleza ukweli wote. 34Yesu akamwambia, “Binti, imani yako imekuponya. Nenda kwa amani, upone kabisa ugonjwa wako.”
Yesu Amfufua Binti Yairo
35Alipokuwa akiongea, watu wakafika kutoka nyumbani kwa Yairo wakamwambia, “Usimsumbue tena mwalimu, binti yako amefar iki. ” 36Lakini Yesu hakuyatilia maanani maneno hayo, akamwam bia Yairo, “Usiogope, bali amini tu.”
37Hakumruhusu mtu mwingine amfuate isipokuwa Petro, Yakobo na Yohana, nduguye Yakobo.
38Walipofika nyumbani kwa yule kiongozi wa sinagogi, Yesu aliona vurugu na watu wengi wakilia na kuomboleza kwa nguvu. 39Alipoingia ndani, aliwaambia, “Kwa nini mnafanya vurugu na kuomboleza? Mtoto hakufariki bali amelala.” 40Wale watu wakam cheka kwa dharau. Lakini yeye akawatoa wote nje, akawachukua baba na mama wa yule mtoto pamoja na wale wanafunzi aliokuwa nao, wakaenda pale alipokuwa yule mtoto. 41Akamwinua mtoto akamwam bia, “Talitha kumi!” Maana yake, “Binti mdogo, nakwambia amka!’ ’
42Mara yule mtoto akasimama, akaanza kutembea. Alikuwa na umri wa miaka kumi na miwili. Walipoona haya, walistaajabu sana. 43Yesu akawaamuru wasimweleze mtu jambo hili, na akawaambia wampe yule mtoto chakula.