Mpango Wa Kumwua Yesu
1Siku mbili tu kabla ya sikukuu ya Pasaka na sherehe ya mikate isiyotiwa chachu, makuhani wakuu na walimu wa sheria wali kuwa wakitafuta njia ya kumkamata Yesu kwa siri na kumwua. 2Wakaambiana, “Jambo hili tusilifanye wakati wa sikukuu maana watu wanaweza kufanya ghasia.”
Yesu Apakwa Manukato
3Yesu alikuwa Bethania nyumbani kwa Simoni ambaye aliwahi kuwa na ukoma. Alipokuwa mezani akila chakula cha jioni, mwanamke mmoja aliingia ndani akiwa na chupa ya alabasta yenye manukato ya nardo safi ya thamani kubwa. Akaivunja hiyo chupa, akammiminia Yesu manukato hayo kichwani. 4Baadhi ya watu waliokuwapo wali chukia wakasema, “Kwa nini anapoteza bure manukato hayo? 5Si afadhali yangeliuzwa kwa dinari zaidi ya mia tatu na fedha hizo wakapewa maskini?” Wakamkemea huyo mama kwa hasira. 6Lakini Yesu akawaambia, “Kwa nini mnamnyanyasa? Mwacheni! Amenitendea jambo zuri na jema. 7Maskini mnao wakati wote na mnaweza kuwapa tia msaada wakati wo wote mtakapo. Lakini hamtakuwa nami wakati wote. 8Huyu mama amenitendea lile aliloweza. Amenipaka manukato kuniandaa kwa mazishi yangu. 9Nawaambieni hakika, mahali po pote duniani ambapo Habari Njema itahubiriwa, jambo hili alilo nitendea huyu mama, litatajwa kwa ukumbusho wake.”
Yuda Anapanga Kumsaliti Yesu
10Kisha Yuda Iskariote, mmoja wa wale wanafunzi kumi na wawili, akaenda kwa makuhani wakuu kuwaambia kuwa yuko tayari kuwasaidia wamkamate Yesu. 11Walifurahishwa sana na habari hizi, wakaahidi kumlipa fedha. Kwa hiyo yeye akaanza kutafuta nafasi nzuri ya kumsaliti.
Yesu Anakula Pasaka Na Wanafunzi Wake
12Siku ya kwanza ya sherehe ya Mikate isiyotiwa chachu siku ambayo kondoo wa Pasaka huchinjwa, wanafunzi wake walimwuliza Yesu, “Unapenda tukuandalie wapi chakula cha Pasaka?” 13Aka watuma wanafunzi wawili akawaagiza, “Nendeni mjini. Huko mtaku tana na mwanamume amebeba mtungi wa maji. Mfuateni, 14na pale atakapoingia, mwambieni mwenye nyumba, ‘Mwalimu anasema hivi, kiko wapi chumba ambamo nitakula Pasaka pamoja na wanafunzi wangu?’ 15Atawaonyesha chumba kikubwa ghorofani kilichopangwa tayari. Tuandalieni humo.” 16Wale wanafunzi walikwenda mjini wakakuta kila kitu kama alivyowaambia; wakaandaa chakula cha Pasaka. 17Ilipofika jioni, Yesu akaja pamoja na wanafunzi wake kumi na wawili. 18Walipokuwa mezani wakila, akawaambia, “Ninawaam bia hakika, mmoja wenu anayekula pamoja nami, atanisaliti.” 19Wote wakasikitika. Wakamwuliza mmoja mmoja, “Ni mimi, Bwana?” 20Akawajibu, “Ni mmoja wenu kumi na wawili, yule anayechovya kipande chake cha mkate kwenye bakuli pamoja nami. 21Mimi Mwana wa Adamu sina budi kufa kama maandiko yasemavyo. Lakini ole wake yeye atakayenisaliti. Ingelikuwa heri kama hakuz aliwa!”
Chakula Cha Bwana
22Walipokuwa wakila, Yesu akachukua mkate, akashukuru , akaumega akawapa wanafunzi wake akisema, “Pokeeni, huu ni mwili wangu.” 23Kisha akachukua kikombe, akashukuru, akawapa, wote wakanywa humo. 24Akawaambia, “Hii ni damu yangu ya agano, inayomwagwa kwa faida ya wengi. 25Nawaambieni hakika, sita kunywa tena divai mpaka siku ile nitakapokunywa divai mpya katika Ufalme wa Mungu.”
26Walipokwisha kuimba wimbo walikwenda kwenye mlima wa
Yesu Atabiri Kuwa Petro Atamkana
28Yesu akawaambia, “Ninyi nyote mtakimbia mniache kwa maana imeandikwa: ‘Nitampiga mchungaji na kondoo watatawanyika.’ 29Lakini nikisha fufuka nitawatangulia kwenda Galilaya. 30Petro akasema, “Hata kama wengine wote watakuacha, mimi sitakuacha.” Yesu akamwambia, “Ninakwambia hakika, usiku huu huu, kabla jogoo hajawika mara mbili, utakanusha mara tatu kwamba hunifahamu.” 31Lakini Petro akasisitiza, “Hata kama ni lazima niuawe pamoja nawe, sitakukana.” Na wale wanafunzi wen gine wote wakasema hivyo hivyo.
Yesu Anasali Bustanini Gethsemane
32Wakafika mahali paitwapo Gethsemane, Yesu akawaambia wanafunzi wake, “Kaeni hapa wakati mimi naomba.” 33Kisha aka wachukua Petro na Yakobo na Yohana. Akawa na huzuni na uchungu mwingi. 34Akawaambia, “Moyo wangu umejaa huzuni kiasi cha kufa; kaeni hapa mkeshe.” 35Akaenda mbele kidogo, akajitupa chi ni akaomba kuwa kama ikiwezekana saa hiyo ya mateso aiepuke. 36Akasema, “Aba, Baba, mambo yote yawezekana kwako. Tafadhali niondolee kikombe hiki cha mateso. Lakini si kama nitakavyo mimi, bali mapenzi yako yatimizwe.” 37Akarudi, akakuta wame lala. Akamwambia Petro, “Simoni, umelala? Hukuweza kukesha hata kwa saa moja? 38Kesheni na kuomba msije mkaingia katika majar ibu. Roho i radhi lakini mwili ni dhaifu.” 39Akaondoka tena akaenda kuomba akisema maneno yale yale. 40Aliporudi tena ali wakuta wanafunzi wake wamelala; macho yao yalikuwa mazito na hawakujua la kumwambia. 41Aliporudi mara ya tatu aliwaambia, “ Bado mmelala na kupumzika? Imetosha! Saa imefika. Mimi Mwana wa Adamu ninatiwa mikononi mwa wenye dhambi. 42Amkeni twendeni, tazameni, yule ambaye amenisaliti amekaribia.”
Yesu Akamatwa
43Yesu alipokuwa bado anazungumza, Yuda, mmoja wa wale wanafunzi kumi na wawili, akafika pamoja na umati wa watu wenye mapanga na marungu. Watu hao walikuwa wametumwa na makuhani wakuu, waandishi, na wazee. 44Yuda, yule msaliti, alikuwa amewapa ishara wale watu kuwa, “Yule nitakayembusu, ndiye mnayemtaka, mkamateni na kumchukua akiwa chini ya ulinzi.”
45Kwa hiyo Yuda alipofika, alimwendea Yesu akamwambia, “Mwalimu,” akambusu. 46Wakamkamata Yesu, wakamweka chini ya ulinzi. 47Lakini mmoja wa wale waliokuwa wamesimama hapo aka chukua upanga akampiga mtumishi wa kuhani mkuu, akamkata sikio. 48Kisha Yesu akasema, “Mbona mmekuja kunikamata kwa mapanga na marungu? Kwani mimi ni jambazi? 49Siku zote nilikuwa pamoja nanyi nikifundisha Hekaluni wala hamkunikamata. Lakini Maandiko lazima yatimie. ” 50Ndipo wanafunzi wake wote wakamwacha, wakakimbia. 51Kijana mmoja aliyekuwa amevaa shuka tu alikuwa akimfuata Yesu. Walipomkamata, 52alikimbia uchi, akaacha shuka lake.
Yesu Afikishwa Barazani
53Kisha wakampeleka Yesu nyumbani kwa kuhani mkuu ambapo makuhani wakuu, wazee, na walimu wa sheria walikuwa wamekuta nika. 54Petro aliwafuata kwa mbali, akaingia barazani kwa kuhani mkuu, akaketi pamoja na walinzi akiota moto. 55Makuhani wakuu na wajumbe wote wa Baraza walijaribu kutafuta ushahidi wa kumshtaki Yesu ili wapate kumwua, lakini hawakupata. 56Wengi walitoa ushahidi wa uongo, lakini ushahidi wao haukupatana.
57Ndipo watu fulani wakasimama wakatoa ushahidi wa uongo wakisema, 58“Sisi tulimsikia akisema, ‘Mimi nitabomoa Hekalu hili lililojengwa na wanadamu, na katika siku tatu nitajenga lin gine ambalo halikujengwa na wanadamu.’ ” 59Lakini hata hawa, ushahidi wao ulipingana.
60Kuhani Mkuu akasimama mbele ya Baraza akamwuliza Yesu, “Huwezi kujibu mashtaka haya ambayo watu hawa wameleta juu yako?” 61Lakini Yesu alikaa kimya; hakusema neno lo lote. Kuhani Mkuu akamwuliza, “Wewe ndiye Kristo, Mwana wa Mungu Mtu kufu?” 62Yesu akajibu, “Mimi ndiye, na mtaniona mimi Mwana wa Adamu nimeketi upande wa kulia wa Mungu Mwenyezi, na nikija na mawingu ya mbinguni.”
63Kuhani Mkuu akararua mavazi yake, akasema, “Tuna haja gani tena ya mashahidi? 64Ninyi wote mmemsikia akikufuru! Mna toa hukumu gani?” Wote wakamhukumu kwamba ana hatia na auawe.
65Kisha baadhi ya watu wakaanza kumtemea mate; wakamfunga kitambaa usoni wakampiga na kumwambia, “Toa unabii, utuambie nani amekupiga!” Maaskari wakampokea kwa mapigo.
Petro Amkana Yesu
66Petro alikuwa bado yuko barazani. Kisha akaja mtumishi mmoja wa kike wa kuhani mkuu. 67Alipomwona Petro akiota moto, alimtazama sana, akamwambia, “Wewe pia ulikuwa pamoja na Yesu Mnazareti.” 68Lakini Petro akakataa, akasema, “Sijui wala sielewi unalosema,” akaondoka akaenda mlangoni. 69Yule mtumi shi wa kike akamwona, akawaambia tena wale waliokuwa wamesimama pale, “Huyu mtu ni mmoja wao.” 70Lakini Petro akakana tena. Baada ya muda kidogo wale waliokuwa wamesimama hapo pamoja naye wakamwambia, “Hakika wewe ni mmoja wao, kwa maana wewe pia ni Mgalilaya!” 71Petro akaanza kulaani na kuapa, akawaambia, “Simjui huyo mtu mnayemsema.”
72Hapo hapo jogoo akawika mara ya pili. Petro akakumbuka lile neno ambalo Yesu alikuwa amemwambia, “Kabla jogoo hajawika mara mbili, utanikana mara tatu.” Akalia kwa uchungu. Pilato Anamhoji Yesu