1Yesu akaendelea kuwaambia, ‘ ‘Ninawahakikishia kuwa wapo watu hapa ambao hawatakufa kabla ya kuuona Ufalme wa Mungu ukija kwa nguvu.”
Yesu Ageuka Sura
2Baada ya siku sita, Yesu aliwachukua Petro, Yakobo na Yohana akawapeleka juu ya mlima mrefu ambapo walikuwa faraghani, peke yao. Na huko, wakiwa wanamtazama, Yesu akageuka sura. 3Mavazi yake yakametameta kwa weupe, yakang’aa, yakawa meupe kuliko ambavyo dobi ye yote duniani angaliweza kuyang’aarisha. 4Musa na Eliya wakawatokea nao walikuwa wakizungumza na Yesu.
5Petro akamwambia Yesu , “Mwalimu, ni vizuri kwamba sisi tuko hapa. Tutengeneze vibanda vitatu: kimoja chako, kimoja cha Musa na kingine cha Eliya.” 6Petro hakujua aseme nini kwa maana yeye na wenzake walikuwa wameogopa sana.
7Ndipo pakatokea wingu, likawafunika, na sauti kutoka katika wingu hilo ikasema, “Huyu ni mwanangu nimpendaye, msikilizeni yeye.” 8Mara walipotazama huku na huku hawakuona mtu mwingine tena isipokuwa Yesu.
9Walipokuwa wakiteremka mlimani, Yesu akawakataza wasim wambie mtu ye yote mambo waliyoona, mpaka yeye Mwana wa Mungu atakapofufuka kutoka kwa wafu. 10Wakatii agizo hilo, lakini wakawa wanajadiliana kati yao maana ya ‘Kufufuka kutoka kwa wafu.’ 11Wakamwuliza, “Kwa nini walimu wa sheria husema kwamba ni lazima Eliya aje kwanza kabla mambo haya hayajatokea?’ ’ 12Yesu akawajibu, “Ni kweli, Eliya anakuja kwanza kusawazisha mambo yote. Hata hivyo, mbona imeandikwa kwamba Mimi, Mwana wa Adamu ni lazima niteseke sana na kudharauliwa? 13Lakini nina waambia, Eliya amekwisha kuja na wamemtendea walivyopenda, kama Maandiko yasemavyo juu yake.”
Yesu Amponya Mvulana Mwenye Pepo
14Walipowafikia wale wanafunzi wengine, waliwakuta wame zungukwa na umati mkubwa wa watu na baadhi ya walimu wa sheria wakibishana nao. 15Mara wale watu walipomwona Yesu, walistaaj abu sana, wakamkimbilia, wakamsalimu. 16Akawauliza wanafunzi wake, “Mnabishana nini nao?”
17Mtu mmoja katika ule umati wa watu akajibu, “Mwalimu, nimemleta kwako mtoto wangu wa kiume kwa maana amepagawa na pepo ambaye amemfanya kuwa bubu. 18Kila mara pepo huyo amwingiapo mwanangu, humwangusha chini na kumfanya atokwe povu mdomoni na kusaga meno, kisha mwili wake hukauka. Nimewaomba wanafunzi wako wamtoe pepo huyo, lakini hawakuweza.”
19Yesu akawaambia, “Ninyi kizazi kisicho na imani! Nita kuwa nanyi mpaka lini? Nitawavumilia mpaka lini? Mleteni huyo mtoto kwangu!” 20Wakamleta. Yule pepo alipomwona Yesu, alimtia yule mvulana kifafa, akaanguka chini akajiviringisha viringisha huku akitokwa na povu mdomoni. 21Yesu akamwuliza baba yake, “Mwanao amekuwa na hali hii tangu lini?” Akamjibu, “Tangu utoto wake. 22Na mara nyingi huyo pepo amemwangusha kwenye moto au kwenye maji ili kuangamiza maisha yake. Lakini kama wewe unaweza kufanya cho chote, tafadhali tuonee huruma, utusaidie.” 23Yesu akasema, “Kama unaweza! Kila kitu kinawezekana kwa mtu mwenye imani.” 24Ndipo yule baba akasema kwa sauti, “Ninaamini. Nisaidie niweze kuamini zaidi!” 25Naye Yesu ali poona umati wa watu unazidi kusongana kuja hapo walipokuwa, akam kemea yule pepo mchafu akisema, “Wewe pepo bubu na kiziwi, naku amuru umtoke, usimwingie tena!” 26Yule pepo akapiga kelele, akamtia kifafa kwa nguvu kisha akatoka. Yule mvulana alionekana kama amekufa; kwa hiyo watu wengi wakasema, “Amekufa.” 27Lakini Yesu akamshika mkono akamwinua, naye akasimama.
28Walipokwisha kuingia ndani ya nyumba, wanafunzi wake wakamwuliza wakiwa peke yao, “Mbona sisi hatukuweza kumtoa huyo pepo?” 29Yesu akawajibu, “Pepo wa aina hii hawezi kutoka isi pokuwa kwa maombi.”
Yesu Azungumzia Tena Kifo Chake
30Wakaondoka mahali hapo, wakapitia Galilaya. Yesu haku taka mtu ye yote afahamu walipokuwa 31kwa maana alikuwa anawa fundisha wanafunzi wake. Alikuwa akiwaambia, “Mimi Mwana wa Adamu nitasalitiwa mikononi mwa watu ambao wataniua, lakini siku ya tatu baada ya kuuawa, nitafufuka.” 32Lakini wao hawakuelewa alichokuwa akisema na waliogopa kumwuliza.
Mabishano Kuhusu Aliye Mkuu
33Basi wakafika Kapernaumu na baada ya kuingia nyumbani akawauliza, “Mlikuwa mnabishana nini njiani?” 34Lakini hawa kumjibu, kwa sababu njiani walikuwa wakibishana kuhusu nani kati yao alikuwa mkuu zaidi.
35Akaketi chini, akawaita wote kumi na wawili akawaambia: “Mtu anayetaka kuwa kiongozi hana budi kuwa wa chini kuliko wote na kuwa mtumishi wa wote.” 36Kisha akamchukua mtoto mdogo akamweka mbele yao, akamkumbatia akawaambia, 37“Mtu ye yote amkaribishaye mmoja wa hawa watoto wadogo, ananikaribisha mimi. Na ye yote anayenikaribisha mimi anamkaribisha Baba yangu ali yenituma.”
Kutumia Jina La Yesu
38Yohana akamwambia, “Mwalimu, tumemwona mtu akitoa pepo kwa jina lako tukamzuia kwa sababu yeye si mmoja wetu.” 39Yesu akasema, “Msimzuie, ye yote atendaye miujiza kwa jina langu kwani hawezi kunigeuka mara moja na kunisema vibaya. 40Kwa maana ye yote ambaye si adui yetu yuko upande wetu. 41Ninawahakikishia kwamba mtu atakayewapa japo maji ya kunywa kwa kuwa ninyi ni wafuasi wangu, atapewa tuzo.”
Kuhusu Kuwakwaza Wengine
42“Na mtu atakayesababisha mmojawapo wa hawa wadogo waniaminio kupoteza imani yake, ingalikuwa nafuu kama mtu huyo angefungiwa jiwe kubwa shingoni akatupwa ziwani. 43Kama mkono wako ukikusababisha utende dhambi, ukate. Ni afadhali kuingia katika uzima ukiwa na mkono mmoja kuliko kuwa na mikono miwili ukaingia katika moto usiozimika. [ 44Huko funza hawafi wala moto hauzimiki.] 45Na kama mguu wako ukikusababisha utende dhambi, ukate. Ni afadhali kuingia katika uzima ukiwa kiwete kuliko kuwa na miguu miwili ukaingia katika moto usiozimika. [ 46Huko funza hawafi wala moto hauzimiki.] 47Na kama jicho lako litakusababisha utende dhambi, ling’oe. Ni afadhali kuwa chongo ukaingia katika Ufalme wa Mungu kuliko kuwa na macho mawili ukatupwa Jehena. 48Huko funza hawafi wala moto hauzimiki. 49Wote watatiwa chumvi kwa moto. 50“Chumvi ni nzuri, lakini ikipoteza ladha yake utafanya nini ili iweze kukolea tena? Muwe na chumvi ndani yenu. Muishi pamoja kwa amani.”