Marko 4

Mfano Wa Mbegu

1Wakati mwingine tena Yesu alianza kufundisha kando ya ziwa. Watu wengi walikusanyika wakasongamana mpaka ukingoni mwa ziwa. Ikambidi Yesu aingie kwenye mashua, akaketi humo. 2Akawafundisha mambo mengi kwa kutumia mifano na katika mafundisho yake akasema:

3“Sikilizeni! Mkulima mmoja alikwenda kupanda mbegu zake. 4Alipokuwa akipanda, baadhi ya mbegu zilianguka njiani; ndege wakaja wakazila. 5Nyingine zilianguka kwenye mwamba ambapo kuli kuwa na udongo haba; zikaota haraka. Kwa kuwa udongo haukuwa na kina, 6jua kali lilipowaka zilinyauka na kukauka kwa kuwa hazi kuwa na mizizi. 7Mbegu nyingine zilianguka kwenye miiba, miiba hiyo ikakua ikazisonga kwahiyo hazikuzaa matunda.

8Na mbegu nyingine zilianguka kwenye udongo mzuri, zikaota vizuri na kukua; zikazaa matunda; moja thelathini, nyingine sitini na nyingine mia moja.” 9Kisha Yesu akasema, “Mwenye nia ya kusikia na asikie.”

Kwa Nini Yesu Alitumia Mifano

10Alipokuwa peke yake, baadhi ya wale waliokuwepo, pamoja na wanafunzi wake kumi na wawili, walimwuliza kuhusu mifano yake. 11Akawaambia, “Siri ya Ufalme wa Mungu imefunuliwa kwenu, lakini kwa wale walioko nje ya Ufalme wa Mungu, kila kitu husemwa kwa mifano 12ili: ‘Kutazama watazame lakini wasione, kusikia wasikie lakini wasielewe. Kwa maana kama wangesikia na kuelewa wangegeuka na kutubu, wakasamehewa.’ ”

Yesu Afafanua Maana Ya Mfano Wa Mbegu

13Kisha Yesu akawauliza, “Hamwelewi maana ya mfano huu? Mtaelewaje basi mifano mingine? 14Yule mtu aliyepanda mbegu, alipanda neno la Mungu. 15Mbegu zilizoanguka njiani ni sawa na watu ambao husikia neno la Mungu na shetani akaja mara moja na kulichukua lile neno lililopandwa ndani yao. 16Hali kadhalika, mbegu iliyoanguka kwenye mwamba ni sawa na watu ambao hulisikia neno na kulipokea kwa furaha. 17Lakini kwa kuwa neno halipenyi ndani, linadumu kwa muda mfupi. Taabu au mateso yanapotokea kwa ajili ya hilo neno, wao hupoteza imani yao. 18Na wengine, ni kama mbegu zile zilizoanguka kwenye miiba. Wao hulisikia neno, 19lakini mahangaiko ya dunia, udanganyifu wa mali na tamaa za mambo mbalimbali hulisonga lile neno, lisizae matunda.

20“Bali wengine ni kama ile mbegu iliyopandwa kwenye udongo mzuri. Wao hulisikia neno wakalipokea na kuzaa matunda: wengine thelathini, wengine sitini, na wengine mia moja.”

Mfano Wa Taa

21Akawaambia tena, “Je, mtu anapowasha taa, huifunika kwa bakuli au kuiweka mvunguni? Si anaiweka mahali pa wazi? 22Hali kadhalika, kila kilichofichwa kitatolewa hadharani; na kila siri itafichuliwa. 23Mwenye nia ya kusikia, na asikie.”

24Akaendelea kuwaambia, “Myaweke maanani haya mnayosikia. Kipimo mnachotumia kwa wengine ndicho kitakachotumiwa kuwapima na ninyi, hata na zaidi. 25Kwa maana aliye na kitu ataongezewa, na asiye na kitu atanyang’anywa hata kile kidogo alicho nacho.”

Mfano Wa Jinsi Mbegu Inavyoota

26Akawaambia tena, “Ufalme wa mbinguni unafanana na mtu apandaye mbegu shambani. 27Akishazipanda, usiku hulala na mchana huamka, wakati huo mbegu huota na kukua pasipo yeye kujua inakuaje. 28Udongo wenyewe huwezesha mimea hiyo kuchipua, kukua na kukomaa. 29Mavuno yanapokuwa tayari, bila kupoteza wakati, yule mkulima huleta mtu akaikata hiyo mimea kwa kuwa wakati wa kuvuna umefika.”

Mfano Wa Mbegu Ya Haradali

30Akawaambia tena, “Tuufananishe Ufalme wa Mungu na nini? Au tutumie mfano gani ili kuuelezea? 31Tunaweza kuufa nanisha na punje ya haradali, ambayo ni mbegu ndogo sana kuliko mbegu zote zinazopandwa ardhini. 32Lakini ikishaota, hukua ikawa mmea mkubwa kuliko yote katika bustani, ikawa na matawi makubwa hata ndege wa angani wakaweza kujenga viota kwenye kiv uli chake.”

33Yesu alitumia mifano mingine mingi kama hii kuwaelezea neno la Mungu, kwa kadiri walivyoweza kuelewa. 34Hakuwafundisha lo lote kuhusu Ufalme wa Mungu pasipo kutumia mifano. Lakini ali pokuwa na wanafunzi wake, aliwafafanulia kila kitu.

Yesu Atuliza Dhoruba

35Siku hiyo, ilipokaribia jioni, aliwaambia wanafunzi wake, “Tuvuke, twende ng’ambo ya pili.” 36Wakawaacha wale watu wakaingia katika ile mashua ambamo Yesu alikuwa amekaa. Pia palikuwa na mashua nyingine.

37Pakatokea dhoruba kali, mawimbi yakaipiga ile mashua waliyokuwa wakivukia, ikaanza kujaa maji. Yesu alikuwa amelala akiegemea mto sehemu ya nyuma kwenye ile mashua. 38Wanafunzi wake wakamwamsha, wakamwambia, “Mwalimu, hujali kwamba tuna zama?’ 39Akaamka, akaukemea ule upepo, akaiambia ile bahari, “Kaa kimya! Tulia!” Ule upepo ukatulia, kukawa shwari.

40Yesu akawaambia wanafunzi wake, “Kwa nini mnaogopa? Je, bado hamna imani?”

41Lakini wao walikuwa wamejawa na hofu wakaulizana, “Ni nani huyu ambaye hata upepo na mawimbi vinamtii?”