Mgawanyiko Katika Kanisa
1Lakini ndugu zangu, mimi sikuweza kusema nanyi kama watu wa kiroho, bali kama watu wa mwili, na kama watoto wachanga katika Kristo. 2 Niliwalisha maziwa, sio chakula kigumu; kwa kuwa mli kuwa hamjawa tayari kukipokea. 3 Kwa maana ninyi bado mnatawaliwa na mambo ya mwili. Je, wakati kuna wivu na kugombana kati yenu, ninyi si watu wa mwili wenye tabia kama za watu wa kawaida? 4 Kwa maana mmoja anaposema, “Mimi ni wa Paulo,” na mwingine, “Mimi ni wa Apolo” hamfanyi kama watu wa kawaida?
5 Hata hivyo, Apolo ni nani? Na Paulo ni nani? Sisi ni watum ishi tu ambao kama Bwana alivyotupangia kila mmoja kazi yake, mliamini kwa msaada wetu. 6 Mimi nilipanda mbegu, na Apolo akaimwagilia maji, lakini ni Mungu aliyefanya mbegu iote. 7 Kwa hiyo anayepanda mbegu na anayemwagilia maji si kitu, bali Mungu pekee ndiye aliyefanya mbegu iote. 8 Anayepanda mbegu ni sawa na yule anayemwagilia maji. Kila mmoja wao atapokea malipo yake kulingana na kazi yake. 9 Sisi ni wafanyakazi pamoja na Mungu; ninyi ni shamba la Mungu; ninyi ni jengo la Mungu.
10 Kwa neema niliyopewa na Mungu nilijenga msingi kama mjenzi hodari, na mtu mwingine ana jenga juu ya msingi huo. Lakini kila mmoja awe mwangalifu anavyojenga juu yake. 11 Kwa maana hakuna mtu anayeweza kuweka msingi mwingine isipokuwa ule uliokwisha jengwa, ambao ni Yesu Kristo. 12 Kama mtu ye yote atajenga juu ya msingi huu akitumia dhahabu, fedha, mawe ya tha mani, mbao, majani au nyasi, 13 kazi yake itaonekana; kwa kuwa ile siku itaidhihirisha kazi yake. Itadhihirishwa kwa moto, na moto utapima ubora wa kazi ya kila mtu. 14 Kama alichojenga hakitaharibiwa kwa moto, atapokea tuzo. 15 Kama kazi ya mtu itateketea, atapata hasara, ila yeye mwenyewe ataokolewa, lakini kama mtu aliyenusurika kwenye moto.
16 Je, hamjui kwamba ninyi ni Hekalu la Mungu, na kwamba Roho wa Mungu anakaa ndani yenu? 17 Kama mtu ye yote akiliharibu Hekalu la Mungu, Mungu atamharibu mtu huyo. Kwa sababu Hekalu la Mungu ni takatifu, na ninyi ni Hekalu hilo. 18 Mtu asijidanganye mwenyewe. Kama kuna mtu miongoni mwenu anadhani kuwa yeye ana hekima kwa kipimo cha nyakati hizi, basi afadhali awe mjinga ili apate kuwa na hekima ya kweli. 19 Kwa maana hekima ya ulimwengu huu ni upuuzi mbele za Mungu. Kama Maandiko yasemavyo, “Mungu huwanasa wenye hekima katika hila yao.’ ’ 20 Na tena, “Bwana anajua kwamba mawazo ya wenye hekima ni bure.”
21 Kwa hiyo mtu asijivune kwa sababu ya watu. Kwa kuwa vitu vyote ni vyenu, 22 kama ni Paulo au Apolo au Petro au dunia au maisha au kifo, au wakati uliopo au wakati unaokuja, haya yote ni yenu; 23 na ninyi ni wa Kristo, na Kristo ni wa Mungu.