Ujumbe Wa Msalaba
1Nilipokuja kwenu ndugu zangu, sikuja kuhubiri siri ya mpango wa Mungu kwa kutumia ufasaha wa kuzungumza au hekima ya binadamu.
2 Kwa kuwa niliamua kwamba wakati nikiwa nanyi nitasahau kila kitu isipokuwa Yesu Kristo; Kristo aliyesulubiwa msalabani. 3 Nilikuja kwenu nikiwa mdhaifu, mwenye woga na nikitetemeka sana. 4 Kuhubiri kwangu na ujumbe wangu haukuwa na hekima na maneno ya kuwashawishi watu, bali ujumbe wangu ulidhihirisha wazi nguvu za Roho, 5 ili imani yenu isiwe imejengwa katika hekima ya wanadamu bali ijengwe katika nguvu ya Mungu.
Hekima Ya Mungu
6 Lakini miongoni mwa watu waliokua kiroho, tunafundisha maneno ya hekima, hii si hekima ya ulimwengu huu au ya watawala wa nyakati hizi ambao watatoweka. 7 Hekima tunayofundisha ni hekima ya siri ya Mungu ambayo imefichwa kwa wanadamu, na ambayo Mungu aliipanga kabla ulimwengu kuwepo, kwa ajili ya utukufu wetu. 8 Watawala wa nyakati zetu hawakuielewa hekima hii. Kwa maana kama wangeliijua, wasingalimsulubisha Bwana wa Utukufu.
9 Lakini, kama Maandiko yasemavyo, “Hakuna aliyeona, hakuna aliyesikia, hakuna aliyewaza, kile ambacho Mungu amekiandaa kwa ajili ya watu wampendao.” 10 Lakini Mungu amekidhihirisha kwetu kwa njia ya Roho wake. Roho huchunguza kila kitu, hata mambo ya ndani ya Mungu. 11 Kwa maana ni nani anajua mawazo ya mtu isipo kuwa roho aliye ndani ya huyo mtu? Vivyo hivyo hakuna mtu anayeelewa mawazo ya Mungu isipokuwa Roho wa Mungu. 12 Sisi hat ukupokea roho ya dunia hii bali Roho aliyetoka kwa Mungu ili tuweze kuelewa yale ambayo Mungu ametupatia bure. 13 Haya ndio tunayozungumzia, lakini si kwa maneno tuliyofundishwa na hekima ya wanadamu bali kwa maneno tuliyofundishwa na Roho, nasi tunafa fanua mambo ya kiroho kwa watu wa kiroho. 14 Mtu ambaye hana Roho wa Mungu hawezi kupokea mambo yanayotoka kwa Roho wa Mungu kwa sababu mambo hayo ni upuuzi kwake; na hawezi kuyaelewa kwa kuwa hayo yanaeleweka tu kwa msaada wa Roho.
15 Mtu wa kiroho anao uwezo wa kupima kila kitu, lakini yeye hapimwi na mtu. 16 “Kwa maana ni nani amefahamu mawazo ya Bwana ili apate kumshauri?” Lakini sisi tunayo nia ya Kristo.