1 Wakorintho 3

Mgawanyiko Katika Kanisa

1Lakini ndugu zangu, mimi sikuweza kusema nanyi kama watu wa kiroho, bali kama watu wa mwili, na kama watoto wachanga katika Kristo. 2Niliwalisha maziwa, sio chakula kigumu; kwa kuwa mli kuwa hamjawa tayari kukipokea. 3Kwa maana ninyi bado mnatawaliwa na mambo ya mwili. Je, wakati kuna wivu na kugombana kati yenu, ninyi si watu wa mwili wenye tabia kama za watu wa kawaida? 4Kwa maana mmoja anaposema, “Mimi ni wa Paulo,” na mwingine, “Mimi ni wa Apolo” hamfanyi kama watu wa kawaida?

5Hata hivyo, Apolo ni nani? Na Paulo ni nani? Sisi ni watum ishi tu ambao kama Bwana alivyotupangia kila mmoja kazi yake, mliamini kwa msaada wetu. 6Mimi nilipanda mbegu, na Apolo akaimwagilia maji, lakini ni Mungu aliyefanya mbegu iote. 7Kwa hiyo anayepanda mbegu na anayemwagilia maji si kitu, bali Mungu pekee ndiye aliyefanya mbegu iote. 8Anayepanda mbegu ni sawa na yule anayemwagilia maji. Kila mmoja wao atapokea malipo yake kulingana na kazi yake. 9Sisi ni wafanyakazi pamoja na Mungu; ninyi ni shamba la Mungu; ninyi ni jengo la Mungu.

10Kwa neema niliyopewa na Mungu nilijenga msingi kama mjenzi hodari, na mtu mwingine ana jenga juu ya msingi huo. Lakini kila mmoja awe mwangalifu anavyojenga juu yake. 11Kwa maana hakuna mtu anayeweza kuweka msingi mwingine isipokuwa ule uliokwisha jengwa, ambao ni Yesu Kristo. 12Kama mtu ye yote atajenga juu ya msingi huu akitumia dhahabu, fedha, mawe ya tha mani, mbao, majani au nyasi, 13kazi yake itaonekana; kwa kuwa ile siku itaidhihirisha kazi yake. Itadhihirishwa kwa moto, na moto utapima ubora wa kazi ya kila mtu. 14Kama alichojenga hakitaharibiwa kwa moto, atapokea tuzo. 15Kama kazi ya mtu itateketea, atapata hasara, ila yeye mwenyewe ataokolewa, lakini kama mtu aliyenusurika kwenye moto.

16Je, hamjui kwamba ninyi ni Hekalu la Mungu, na kwamba Roho wa Mungu anakaa ndani yenu? 17Kama mtu ye yote akiliharibu Hekalu la Mungu, Mungu atamharibu mtu huyo. Kwa sababu Hekalu la Mungu ni takatifu, na ninyi ni Hekalu hilo. 18Mtu asijidanganye mwenyewe. Kama kuna mtu miongoni mwenu anadhani kuwa yeye ana hekima kwa kipimo cha nyakati hizi, basi afadhali awe mjinga ili apate kuwa na hekima ya kweli. 19Kwa maana hekima ya ulimwengu huu ni upuuzi mbele za Mungu. Kama Maandiko yasemavyo, “Mungu huwanasa wenye hekima katika hila yao.’ ’ 20Na tena, “Bwana anajua kwamba mawazo ya wenye hekima ni bure.”

21Kwa hiyo mtu asijivune kwa sababu ya watu. Kwa kuwa vitu vyote ni vyenu, 22kama ni Paulo au Apolo au Petro au dunia au maisha au kifo, au wakati uliopo au wakati unaokuja, haya yote ni yenu; 23na ninyi ni wa Kristo, na Kristo ni wa Mungu.