Yohana 2

Yesu Ahudhuria Harusi Mjini Kana

1Siku ya tatu kulikuwa na harusi katika mji wa Kana ulioko Galilaya. Mama yake Yesu alikuwapo 2na Yesu pamoja na wanafunzi wake walikuwa wamealikwa pia. 3Divai ilipowaishia, mama yake Yesu alimwambia, “Hawana divai.” 4Yesu akamjibu, “Mama, mbona unanihusisha kwenye jambo hili? Wakati wangu bado haujafika.” 5Mama yake akawaambia watumishi, “Lo lote atakalowaambia, fanyeni. ” 6Basi ilikuwapo hapo mitungi sita ya kuwekea maji ya kunawa, kufuatana na desturi ya Wayahudi ya kutawadha. Kila mtungi ungeweza kujazwa kwa madebe sita au saba ya maji. 7Yesu akawaambia wale watumishi, “Ijazeni mitungi hiyo maji.” Wakaijaza mpaka juu. 8Kisha akawaambia, “Sasa choteni maji kidogo mumpelekee mkuu wa sherehe.” Wakachota, wakampelekea. 9Yule mkuu wa sherehe akayaonja yale maji ambayo yalikuwa yame geuka kuwa divai. Hakujua divai hiyo imetoka wapi ingawa wale watumishi waliochota yale maji walifahamu. Basi akamwita bwana harusi kando 10akamwambia, “Watu wote huwapa wageni divai nzuri kwanza kisha wakianza kutosheka huwaletea divai hafifu.

Imekuwaje wewe ukaiweka divai nzuri mpaka sasa?”

11Hii ilikuwa ishara ya kwanza aliyofanya Yesu. Muujiza huu ulifanyika katika mji wa Kana huko Galilaya, ambako Yesu alidhi hirisha utukufu wake, na wanafunzi wake wakamwamini. 12Baada ya haya, Yesu pamoja na mama yake, ndugu zake na wanafunzi wake, walikwenda Kapernaumu ambapo alikaa kwa siku chache.

Yesu Alitakasa Hekalu

13Ilipokaribia sikukuu ya Wayahudi iitwayo Pasaka, Yesu alikwenda Yerusalemu. 14Alipoingia Hekaluni aliwakuta watu wakiuza ng’ombe, kondoo na njiwa, na wengine wamekaa kwenye meza zao wakifanya biashara ya kubadilishana fedha. 15Akatengeneza mjeledi wa kamba akawafukuza wote kutoka Hekaluni pamoja na kon doo na ng’ombe; akazipindua meza za wale waliokuwa wakibadilish ana fedha na kuzimwaga fedha zao. 16Akawaambia wale waliokuwa wakiuza njiwa, “Watoeni hapa! Mnathubutuje kuifanya nyumba ya Baba yangu kuwa soko?” 17Wanafunzi wake wakakumbuka kuwa Maan diko yalisema: “Upendo wangu kwa nyumba yako utaniangamiza.”

18Viongozi wa Wayahudi wakamwuliza, “Unaweza kutuonyesha ishara gani kuthibitisha una mamlaka ya kufanya mambo haya?”

19Yesu akawajibu, “Livunjeni hili Hekalu, nami nitalijenga tena kwa siku tatu!”

20Wale Wayahudi wakamjibu, “Hekalu hili lilijengwa kwa muda wa miaka arobaini na sita. Wewe unasema unaweza kulijenga kwa siku tatu?”

21Lakini yeye aliposema ‘Hekalu’ alikuwa anazungumzia mwili wake. 22Kwa hiyo alipofufuliwa kutoka kwa wafu, wanafunzi wake walikumbuka maneno haya; wakayaamini Maandiko na yale maneno ali yosema Yesu.

23Yesu alipokuwa Yerusalemu kwenye sikukuu ya Pasaka, watu wengi waliona ishara za ajabu alizokuwa akifanya, wakamwamini. 24Lakini Yesu hakuwa na imani nao kwa sababu aliwajua binadamu wote. 25Hakuhitaji mtu ye yote amwambie lo lote kuhusu bina damu. Alijua yote yaliyokuwa mioyoni mwao.