Matendo Ya Mitume 21

Paulo Aenda Yerusalemu

1Tulipokwisha agana nao tuliondoka tukasafiri moja kwa moja, mpaka Kosi, na siku ya pili yake tukafika Rodo, na kutoka huko tukaenda Patara. 2Hapo tukapata meli iliyokuwa ikielekea Foinike tukaingia ndani tukasafiri nayo. 3Tulipokaribia kisiwa cha Kipro, tulikizunguka upande wa kushoto, tukasafiri mpaka Siria, tukatia nanga katika bandari ya Tiro ambapo meli yetu ili kuwa ipakue shehena yake. 4Tukawatafuta waamini wa huko, tukakaa nao kwa siku saba. Wale waamini wakiwa wameongozwa na Roho walim wambia Paulo asiende Yerusalemu. 5Muda wa kukaa nao ulipokwisha, tuliendelea na safari yetu na wale ndugu waamini pamoja na wake zao na watoto wao walitusindikiza hadi nje ya mji. Wote tulipiga magoti pale pwani tukaomba, kisha tukaagana.

6Ndipo tukaingia ndani ya meli na wale ndugu wakarudi mak wao. 7Tuliendelea na safari yetu kutoka Tiro tukafika Tolemai, tukawasalimu waamini wa huko na tukakaa nao kwa siku moja. 8Kesho yake tuliondoka tukafika Kaisaria. Huko tukaenda nyumbani kwa mwinjilisti mmoja jina lake Filipo ambaye alikuwa kati ya wale watu saba waliochaguliwa kule Yerusalemu, tukakaa kwake. 9Filipo alikuwa na binti wanne ambao walikuwa bado hawajaolewa nao walikuwa na karama ya unabii. 10Wakati tulipokuwa huko kwa siku kadhaa, alifika nabii mmoja aitwaye Agabo kutoka Yudea. 11Alikuja kutuona akachukua mshipi wa Paulo, akautumia kufunga mikono yake mwenyewe na miguu yake akasema, “Roho Mtakatifu anasema: ‘Hivi ndivyo Wayahudi wa Yerusalemu watakavyomfunga mwe nye mshipi huu na kumkabidhi kwa watu wa mataifa .”’ 12Tulipo sikia maneno haya sisi na ndugu wengine tulimwomba Paulo asiende Yerusalemu. 13Lakini Paulo alijibu, “Kwa nini mnanivunja moyo kwa machozi yenu? Mimi niko tayari kufungwa na hata kufa huko Yerusalemu kwa ajili ya jina la Bwana Yesu.” 14Na kwa kuwa hatukuweza kumshawishi asiende, tuliacha kumsihi tukamwambia, “Mapenzi ya Bwana na yatendeke.”

15Baadaye tulijiandaa tukaondoka kwenda Yerusalemu. 16Baadhi ya waamini kutoka Kaisaria waliongozana nasi, wakat upeleka nyumbani kwa Mnasoni, mtu wa Kipro, mmoja wa waamini wa zamani, tukae kwake.

Taarifa Ya Paulo Kwa Kanisa La Yerusalemu

17Tulipofika Yerusalemu ndugu wa huko walitukaribisha kwa furaha. 18Kesho yake Paulo alikwenda nasi kwa Yakobo, na wazee wote wa kanisa walikuwepo. 19Baada ya kuwasalimu, Paulo alitoa taarifa kamili ya mambo yote ambayo Mungu alifanya kati ya watu wa mataifa kwa kumtumia yeye. 20Baada ya maelezo yake wote walimtukuza Mungu. Ndipo wakamwambia, “Unavyoona ndugu, kuna maelfu ya Wayahudi walioamini; nao wote wanaishika sheria kwa bidii. 21Lakini wamekuwa wakiambiwa habari zako kuwa wewe umew afundisha Wayahudi wanaoishi na watu wa mataifa waache kushika sheria za Musa; na kuwaambia wasitahiri watoto wao, au kufuata mila za Kiyahudi. 22Sasa tufanyeje? Kwa maana watasikia kwamba umefika Yerusalemu. 23Kwa hiyo fanya kama tunavyokushauri. Tunao watu wanne hapa ambao wameweka nadhiri. 24Wachukue hawa ukajitakase pamoja nao na ulipe gharama zao ili wanyoe nywele zao. Kwa njia hii kila mtu atafahamu ya kuwa mambo waliyosikia si ya kweli na kwamba wewe unashika sheria. 25Lakini wale watu wa mataifa walioamini tumewapelekea barua tukiwaambia kuwa tumeamua wajitenge na kitu cho chote ambacho kimetolewa kwanza kama sadaka kwa miungu ya sanamu na wasinywe damu au kula nyama ya mnyama aliyeuawa kwa kunyongwa. Tena ni lazima wajitenge na uasherati.” 26Kwa hiyo Paulo akawachukua wale watu na kesho yake akajita kasa pamoja nao. Akaingia ndani ya Hekalu ili akatoe taarifa ya tarehe ambayo siku zao za utakaso zitamalizika na sadaka kutolewa kwa ajili ya kila mmoja wao.

Paulo Akamatwa

27Zile siku saba zilipokaribia kumalizika, Wayahudi kutoka jimbo la Asia waliokuwa wamemwona Paulo ndani ya hekalu, waka chochea umati mkubwa wa watu wakamkamata Paulo. 28Wakapiga kelele wakasema, “Ndugu Waisraeli, tusaidieni! Huyu ni yule mtu ambaye anafundisha watu kila mahali wawadharau watu wetu, wazid harau sheria zetu na hata hili Hekalu. Zaidi ya hayo amewaleta Wagiriki katika Hekalu na kuchafua hapa mahali patakatifu!” 29Walisema hivi kwa sababu walimwona Trofimo, mwenyeji wa Efeso, akiwa mjini na Paulo wakadhani kuwa Paulo alikuwa amemleta Hekaluni . 30Habari hizi zikawachochea watu wa mji mzima nao wakakimbia pamoja kwa hasira wakamkamata Paulo wakamtoa nje ya Hekalu. Milango ya Hekalu ikafungwa. 31Walipokuwa wakitaka kum wua, habari zikamfikia Jemadari wa jeshi la askari wa Kirumi kwamba Yerusalemu yote ilikuwa katika hali ya machafuko. 32Na mara yule jemadari akachukua maofisa wengine wa jeshi pamoja na maaskari wakakimbilia kwenye ile ghasia. Watu walipomwona jema dari na askari wakija, waliacha kumpiga Paulo. 33Kisha yule jemadari akamkamata Paulo akaamuru afungwe kwa minyororo miwili. Akauliza yeye ni nani na alikuwa amefanya nini. 34Baadhi ya watu wakapiga kelele wakieleza jambo moja na wengine wakieleza jingine. Yule jemadari alipoona kuwa hawezi kupata ukweli kamili kwa sababu ya zile kelele, akaamuru Paulo apelekwe katika ngome ya jeshi. 35Basi walipofika penye ngazi, ilibidi askari wambebe Paulo juu juu kwa sababu ya fujo za ule umati wa watu 36ambao walikuwa wakiwafuata wakipiga kelele, “Mwueni!”

Paulo Anajitetea

37Walipokuwa wanakaribia kuingia katika ngome ya jeshi, Paulo alimwuliza yule jemadari, “Je, naweza kusema jambo moja?” Yule jemadari akajibu, “Kumbe unajua Kigiriki? 38Wewe si yule Mmisri ambaye siku za karibuni alianzisha uasi akaongoza majam bazi elfu nne wenye silaha jangwani?” 39Paulo akajibu, “Mimi ni Myahudi, mzaliwa wa Tarso, jimbo la Kilikia na raia wa mji wenye sifa. Tafadhali niruhusu nizungumze na hawa watu.” 40Yule jemadari alipomruhusu azungumze, Paulo akasimama penye ngazi akawapungia watu mkono ili wanyamaze. Watu walipokuwa kimya kabisa, Paulo akazungumza nao kwa lugha ya Kiebrania, akasema;