Petro Na Yohana Wakamatwa
1Walipokuwa bado wanasema na watu, makuhani, mkuu wa walinzi wa Hekalu na Masadukayo waliwajia wakiwa 2wamekasirika kwa sababu Petro na Yohana walikuwa wakiwafundisha watu kwamba kufu fuka kwa Yesu kunadhihirisha kwamba wafu watafufuka. 3Wakawaka mata wakawaweka jela mpaka kesho yake kwa maana ilikuwa jioni. 4Lakini wengi wa wale waliosikia mahubiri yao waliamini; idadi ya wanaume walioamini ilikuwa kama elfu tano.
5Siku ya pili yake viongozi wa Kiyahudi, wazee na waandishi wa sheria walikusanyika Yerusalemu. 6Walikuwepo Kuhani Mkuu Anasi, Kayafa , Yohana, Aleksanda na ndugu zake Kuhani Mkuu. 7Wakawaleta wale mitume wawili katikati yao wakawauliza, “Ni kwa uwezo gani au mmetumia jina la nani kufanya jambo hili?” 8Petro, akiwa amejawa na Roho Mtakatifu akajibu, “Waheshimiwa viongozi na wazee wa watu, 9kama mnatuhoji kuhusu mambo mema aliyotendewa kilema, na jinsi alivyoponywa, tungependa ninyi na watu wote wa 10Israeli mfahamu kwamba, ni kwa jina la Yesu Kristo wa Nazareti, ambaye ninyi mlimsulubisha lakini Mungu akam fufua kutoka kwa wafu, kwa uwezo wa Yesu, huyu mtu anasimama mbele yenu akiwa mzima kabisa. 11Huyu Yesu ndiye ‘lile jiwe ambalo ninyi wajenzi mlilikataa, ambalo limekuwa jiwe kuu la pembeni.’ 12Wokovu unapatikana kwake tu; kwa maana hakuna jina jingine duniani ambalo wamepewa wanadamu kuwaokoa ila jina la Yesu, na ni kwa jina hilo peke yake tunaweza kuokolewa!”
Ujasiri Wa Petro Na Yohana Washangaza Watu
13Wale viongozi na wazee walipoona ujasiri wa Petro na Yohana na kufahamu ya kuwa walikuwa watu wa kawaida wasio na elimu walishangaa sana. Wakatambua kwamba hawa watu walikuwa na Yesu. 14Lakini kwa kuwa walimwona yule kilema aliyeponywa ame simama nao hawakuweza kusema lo lote kupinga maneno yao. 15Wakawaamuru watoke nje ya ule ukumbi. 16Kisha wakaanza kuulizana, “Tuwafanye nini watu hawa? Hatuwezi kukanusha muujiza huu mkubwa walioufanya ambao ni dhahiri kwa kila mtu Yerusalemu. 17Lakini tunaweza kuzuia jambo hili lisiendelee kuenezwa kwa watu kama tukiwakanya wasiseme tena na mtu ye yote kwa jina la Yesu.” 18Kwa hiyo wakawaita tena ndani wakawaamuru wasiseme au kufundisha watu tena kwa jina la Yesu.
Bora Kumtii Mungu Kuliko Wanadamu
19Ndipo Petro na Yohana wakawajibu, “Ninyi amueni wenyewe lililo bora kutenda mbele za Mungu: kuwatii ninyi au kumtii Mungu. 20Lakini sisi hatuwezi kuacha kusema yale tuliyoyaona na kuyasikia.”
21Wale viongozi wakawaonya tena kwa vitisho, kisha waka waacha waende. Hawakuona njia ya kuwaadhibu kwa kuwa waliwaogopa wale watu ambao walishuhudia ule muujiza uliotendeka, nao wali kuwa wakimsifu Mungu. 22Na yule mtu aliyeponywa alikuwa na umri wa zaidi ya miaka arobaini.
23Mara Petro na Yohana walipoachiliwa, walirudi kwa waamini wenzao wakawaeleza waliyoambiwa na makuhani wakuu na wazee. 24Waamini wote waliposikia maneno yao walimwomba Mungu kwa pamoja wakasema, “Wewe Bwana Mtukufu, uliyeumba mbingu na nchi na bahari na kila kiumbe kilichopo, 25wewe ulitamka kwa njia ya Roho wako mtakatifu kupitia kwa baba yetu Daudi mtumishi wako, aliposema, ‘Mbona mataifa wanaghadhabika, na watu wanawaza mambo yasiyo na maana? 26Wafalme wa dunia wamejiandaa na watawala wamekusanyika wampinge Bwana na Masihi wake.’ 27Ndiyo sababu katika mji huu Herode na Pontio Pilato walikutana na Waisraeli wote na watu wa mataifa juu ya mtumishi wako mtakatifu Yesu, 28wakaamua kumfanyia yale yote ambayo wewe ulikuwa umekusudia tangu awali na kupanga kwa uweza wako yatendeke.
29“Sasa Bwana, sikia vitisho vyao na utuwezeshe sisi wat umishi wako kuhubiri neno lako kwa ujasiri mkuu; 30na unyooshe mkono wako ili tuweze kuponya wagonjwa na kutenda ishara na miu jiza kwa jina la mtumishi wako mtakatifu Yesu.” 31Walipokwisha kusali, nyumba waliyokuwa wamekutania ikatikisika na wote wakaja zwa na Roho Mtakatifu, wakahubiri neno la Mungu kwa ujasiri. 32Waamini wote walikuwa na nia moja na moyo mmoja, wala hakuna aliyeona mali aliyokuwa nayo kuwa yake, bali walishirikiana vitu vyote kwa pamoja. 33Na kwa uwezo mkubwa mitume wakashuhudia kwa ujasiri habari za kufufuka kwa Bwana Yesu. Mungu akawapa wote neema kuu. 34Wala hakuwepo mtu ye yote miongoni mwa waamini aliyepungukiwa na kitu kwa sababu wale waliokuwa na mashamba na nyumba waliuza vyote wakaleta fedha waliyopata 35kwa wale mitume; kila mtu akagawiwa kadiri ya mahitaji yake.
36Ndivyo ilivyokuwa kwamba Yusufu ambaye mitume walimwita Barnaba, maana yake Mwana wa Faraja, wa ukoo wa Lawi kutoka kisiwa cha Kipro 37aliuza shamba alilokuwa nalo akaleta fedha alizopata kwa wale mitume.