Maagizo Kuhusu Ibada
1Basi, kwanza kabisa, naagiza kwamba dua, sala, maombezi na shukrani zitolewe kwa ajili ya watu wote: 2 kwa ajili ya wafalme na wote wenye mamlaka, ili tupate kuishi maisha ya utulivu na amani, tukimcha Mungu na kuwa wenye heshima kwa kila njia. 3 Jambo hili ni jema na linampendeza Mungu Mwokozi wetu 4 ambaye anapenda watu wote waokolewe na wapate kuijua kweli. 5 Maana kuna Mungu mmoja na mpatanishi mmoja kati ya Mungu na wanadamu, yaani mwanadamu Kristo Yesu, 6 aliyejitoa mwenyewe kuwa fidia kwa ajili ya wote. Yeye ni uthibitisho wa mambo haya, uliotolewa kwa wakati wake. 7 Na hii ndio sababu nilichaguliwa niwe mhubiri na mtume, nasema kweli sisemi uwongo; nilichaguliwa niwe mwalimu wa watu wa mataifa katika imani na kweli.
8 Kwa hiyo, nataka kila mahali wanaume wasali wakiinua mikono iliyotakaswa pasipo hasira wala mabishano. 9 Kadhalika, nataka wanawake wajipambe kwa heshima na kwa busara. Mavazi yao yawe nadhifu, si kwa kusuka nywele, kujipamba kwa dhahabu, lulu na mavazi ya gharama kubwa, 10 bali kwa matendo mema kama iwapa savyo wanawake wanaokiri kuwa wanamcha Mungu. 11 Mwanamke na ajifunze katika utulivu na unyenyekevu.
12 Simruhusu mwanamke ye yote kufundisha au kuwa na mamlaka juu ya wanaume. Mwanamke anapaswa kukaa kimya. 13 Kwa maana Adamu aliumbwa kwanza kisha Hawa; 14 na Adamu hakudanganywa bali mwanamke alidanganywa akawa mkosaji. 15 Lakini mwanamke ataoko lewa kwa kuzaa, kama ataendelea kudumu katika imani, upendo na utakatifu, pamoja na kujiheshimu.