Onyo Kuhusu Upendeleo
1Ndugu zangu wapendwa, msiwe na upendeleo mnapoishika imani ya Bwana wetu Yesu Kristo, Bwana wa utukufu. 2 Tuseme mtu mmoja aliyevaa pete ya dhahabu na nguo maridadi anakuja katika mkutano wenu; kisha fukara mmoja mwenye nguo chafu na mbovu akaingia pia. 3 Ikiwa utamshughulikia zaidi yule mtu aliyevaa nguo maridadi ukamwambia, “Keti hapa kwenye kiti kizuri,” lakini yule fukara ukamwambia, “Wewe simama pale,” au “Keti sakafuni, miguuni pangu,” 4 je, hamtakuwa mmefanya ubaguzi mioyoni mwenu na kutoa hukumu itokanayo na mawazo maovu?
5 Sikilizeni, ndugu zangu wapendwa: je, Mungu hakuwachagua wale walio fukara hapa duniani kuwa matajiri wa imani na warithi wa ufalme aliowaahidi wale wampendao? 6 Lakini ninyi mmemvunjia heshima aliye fukara. Je, si matajiri ndio wanaowagandamiza na kuwapelekeni mahakamani? 7 Je, si wao wanaolikufuru jina lile jema mliloitiwa? 8 Kama kweli mnatimiza ile sheria ya kifalme iliyomo katika Maandiko, “Mpende jirani yako kama unavyojipenda mwenyewe,” mnafanya vema. 9 Lakini kama mnafanya ubaguzi, mna tenda dhambi na sheria inawahukumu kuwa ninyi ni wakosaji. 10 Kwa maana mtu ye yote anayetimiza sheria yote isipokuwa akashindwa kutimiza sehemu moja tu, amekuwa na hatia ya kuvunja sheria yote. 11 Kwa sababu yeye aliyesema, “Usizini” ndiye huyo huyo aliyesema, “Usiue.” Kama huzini lakini unaua, umekuwa mvunjaji wa sheria yote.
12 Kwa hiyo semeni na kutenda kama watu watakaohukumiwa kwa sheria iletayo uhuru. 13 Maana hukumu haina huruma kwa mtu asi yekuwa na huruma. Lakini huruma huishinda hukumu.
Imani Na Matendo
14 Kuna faida gani, ndugu zangu, ikiwa mtu atasema, “Ninayo imani,” na huku hana matendo? 15 Tuseme ndugu fulani au dada hana nguo wala chakula. 16 Ikiwa mmoja wenu atawaambia, “Nendeni salama, mkaote moto na kushiba,” pasipo kuwapatia mahitaji yao ya mwili, kuna faida gani? 17 Vivyo hivyo imani peke yake kama haina matendo, imekufa.
18 Lakini mtu mwingine atasema, “Wewe unayo imani; mimi ninayo matendo.” Nionyeshe imani yako pasipo matendo nami nita kuonyesha imani yangu kwa matendo yangu. 19 Unaamini kuwa kuna Mungu mmoja. Vema. Lakini hata mashetani huamini hivyo, nao hutetemeka!
20 Ewe mpumbavu, unataka ushahidi wa kuthibitisha kwamba imani bila matendo ni bure? 21 Je, Abrahamu baba yetu hakuhesa biwa haki kwa matendo, alipomtoa mwanae Isaki madhabahuni? 22 Unaona jinsi ambavyo imani ilitenda kazi pamoja na matendo yake na imani ikakamilishwa kwa matendo. 23 Kwa njia hiyo yaka timizwa yale Maandiko yasemayo, “Abrahamu alimwamini Mungu, na kwa imani yake akahesabiwa kuwa mtu mwenye haki”; naye akaitwa rafiki wa Mungu.
24 Mnaona kwamba mtu huhesabiwa haki kwa matendo wala si kwa imani peke yake. 25 Hali kadhalika Rahabu, yule kahaba, yeye je, hakuhesabiwa haki kwa matendo yake alipowapokea wapelelezi na kuwaambia waende njia nyingine? 26 Kama vile ambavyo mwili pasipo roho umekufa, kadhalika imani pasipo matendo imekufa.