19 1 Yesu akaingia Yeriko, akiwa safarini kuelekea Yerusalemu. 2Hapo, alikuwapo mtu mmoja mkuu wa watoza kodi na pia mtu tajiri, jina lake Zakayo. 3Yeye alitamani sana kumwona Yesu lakini hakuweza kwa sababu ya umati mkubwa wa watu, naye alikuwa mfupi sana. 4Kwa hiyo akatangulia mbio mbele ya umati akapanda juu ya mkuyu ili amwone Yesu ambaye angepitia njia ile. 5Yesu alipofika chini ya huo mkuyu, akatazama juu akamwambia: “Zakayo! Shuka upesi, kwa maana leo nitakuwa mgeni nyumbani kwako!” 6Mara moja Zakayo akashuka, akamkaribisha Yesu nyumbani kwake kwa furaha kubwa. 7Watu wote waliokuwepo, wakaanza kunung’unika, “Amekwenda kuwa mgeni nyumbani kwa mwenye dhambi!” 8Lakini Zakayo akasimama akamwambia Bwana, “Sikia Bwana, nusu ya mali yangu ninaitoa hivi sasa niwagawie maskini, na kama nimemdhulumu mtu ye yote, nitamrudishia mara nne zaidi.” 9Yesu akamwambia, “Leo, wokovu umeingia nyumba hii, kwa sababu huyu naye ni mtoto wa Ibrahimu. 10Kwa maana mimi Mwana wa Adamu nimekuja kutafuta na kuokoa waliopotea.”
Mfano Wa Fedha
11Wakati walipokuwa wanasikiliza haya, Yesu aliendelea kuwaambia mfano. Wakati huo watu walikuwa wakidhani kwamba kwa kuwa walikuwa wanakaribia Yerusalemu, Ufalme wa Mungu ungetokea mara. 12Kwa hiyo akawaambia: “Mtu mmoja wa ukoo wa kitawala, alisafiri kwenda nchi ya mbali ili akapokee madaraka ya kuwa mfalme, kisha arudi. 13Akawaita watumishi wake kumi akawapa kila mmoja fungu la fedha. Akawaambia, ‘Zitumieni kufanyia biash ara mpaka nitakaporudi.’ 14Lakini raia wake walimchukia wakapeleka ujumbe usemao, ‘Hatutaki huyu mtu awe mfalme wetu. ’ 15Hata hivyo alipewa ufalme akarudi nyumbani. Kisha akawaita wale watumishi aliokuwa amewaachia fedha, ili afahamu faida kila mmoja wao aliyopata.
16“Wa kwanza akaja, akasema, ‘Bwana, kutokana na fedha uliyoniachia nimepata faida mara kumi zaidi.’ 17Yule bwana akamjibu, ‘Umefanya vizuri mtumishi mwema! Kwa sababu umekuwa mwaminifu katika wajibu mdogo sana, nakupa mamlaka juu ya miji kumi.’
18“Wa pili naye akaja, akasema, ‘Bwana, fedha yako imeleta faida mara tano zaidi.’ 19Bwana wake akajibu, ‘Nakupa mamlaka juu ya miji mitano.’ 20Kisha akaja mtumishi mwingine akasema, ‘Bwana hii hapa fedha yako. Niliitunza vizuri kwenye kitambaa. 21Nilikuogopa, kwa sababu wewe ni mtu mkali. Unachukua ambapo hukuweka kitu na unavuna mahali ambapo hukupanda kitu.’
22“Bwana wake akamjibu, ‘Nitakuhukumu kwa maneno yako mwe nyewe, wewe mtumishi mwovu ! Kama ulifahamu kwamba mimi ni mtu mkali, nichukuaye mahali ambapo sikuweka kitu na kuvuna ambapo sikupanda; 23kwa nini basi hukuweka fedha zangu benki ili nita kaporudi nizichukue na faida yake?’ 24Ndipo akawaambia wale waliokuwa wamesimama karibu , ‘Mnyang’anyeni fungu lake la fedha mkampe yule mwenye kumi.’ 25Wakamwambia, ‘Bwana, mbona tayari anayo mafungu kumi’? 26Akajibu, ‘Nawahakikishieni kwamba, kila aliye na kitu, Mungu atamwongezea; na yule asiyetumia alicho nacho, atanyang’anywa hata hicho alicho nacho. 27Sasa nileteeni wale maadui zangu ambao hawakutaka mimi niwe mfalme wao; waleteni hapa muwaue mbele yangu.”’
Yesu Aingia Yerusalemu
28Alipokwisha kusema haya, Yesu alikaa mbele ya msafara akielekea Yerusalemu. 29Na alipokaribia Bethfage na Bethania kwenye mlima wa Mizeituni aliwatuma wanafunzi wawili akawaagiza hivi, 30“Nendeni katika kijiji kile kilicho mbele yenu. Mtaka pokuwa mnaingia kijijini, mtamkuta mwana-punda ambaye hajapandwa na mtu bado, amefungwa. Mfungueni, mumlete hapa. 31Kama mtu akiwauliza, ‘Mbona mnamfungua?’ Mwambieni, ‘Bwana anamhitaji.”’
32Wale waliotumwa wakaenda, wakakuta kila kitu kama Yesu alivyokuwa amewaambia. 33Walipokuwa wanamfungua yule mwana- punda wenyewe wakawauliza, “Mbona mnamfungua huyo mwana-punda?” 34Wale wanafunzi wakajibu, “Bwana anamhitaji.” 35Wakamleta kwa Yesu. Wakatandika mavazi yao juu ya huyo mwana-punda, kisha wakampandisha Yesu juu yake. 36Alipokuwa akienda, watu wakatan daza nguo zao barabarani. 37Alipokaribia mteremko wa mlima wa Mizeituni, umati wote wa wanafunzi wake wakaanza kwa sauti kuu kumsifu Mungu kwa furaha kwa ajili ya miujiza yote waliyoiona Yesu akifanya, 38wakasema: “Amebarikiwa Mfalme anayekuja kwa jina la Bwana! Amani mbinguni na Utukufu kwa Mungu.” 39Baadhi ya Mafarisayo waliokuwemo katika umati wakamwambia, “Mwalimu, wanyamazishe wanafunzi wako.” 40Yesu akawajibu, “Nawaambia, hawa wakinyamaza, mawe yatapiga kelele.”
Yesu Anaulilia Mji Wa Yerusalemu
41Alipokaribia Yerusalemu, akauona mji, aliulilia,
42akasema, “Laiti ungalijua leo jinsi ya kupata amani! Lakini sasa huoni! 43Kuna siku ambapo maadui zako watakuzungushia ukuta na kukuzingira na kukushambulia kutoka kila upande. 44Watakutupa chini wewe na wanao ndani ya kuta zako na hawataacha hata jiwe moja juu ya jingine. Hii ni kwa sababu hukutaka kutambua wakati
Yesu Aingia Hekaluni
45Ndipo akaingia Hekaluni akaanza kuwafukuza wale wal iokuwa wakifanya biashara humo. 46Akawaambia, “Imeandikwa katika Maandiko, ‘Nyumba yangu itakuwa nyumba ya sala.’ Lakini ninyi mmeigeuza kuwa pango la wanyang’anyi.”
47Kila siku alikuwa akifundisha Hekaluni. Makuhani wakuu na walimu wa sheria wakiungwa mkono na viongozi wengine walijaribu kila njia wapate kumwua 48lakini hawakupata nafasi kwa sababu watu wote waliomfuata waliyasikiliza maneno yake kwa makini na kuyazingatia. Yesu Aulizwa Kuhusu Mamlaka Yake