1 Wakorintho 16

Matoleo Kwa Ajili Ya Waamini

1Na sasa kuhusu matoleo kwa ajili ya kuwasaidia watu wa Mungu. Kama nilivyoagiza makanisa ya Galatia, fanyeni vivyo hivyo. 2Siku ya kwanza ya juma kila mmoja wenu atenge kiasi cha fedha, kulingana na mapato yake, na fedha hiyo aiweke ili nitaka pokuja pasiwepo na haja ya kufanya mchango. 3Nikishafika nita wapa wale mtakaowachagua barua za kuwatambulisha, ili waweze kupeleka zawadi yenu Yerusalemu. 4Kama ikionekana ni vyema na mimi niende, basi hao watu watafuatana nami.

Mipango Ya Paulo

5Baada ya kupitia Makedonia, nitakuja kwenu; maana natazamia kupitia Makedonia. 6Pengine nitakaa nanyi kwa muda, au hata nitakaa nanyi kipindi chote cha baridi, ili muweze kunisaidia katika safari zangu, po pote niendapo. 7Kwa maana sipendi niwaone sasa nikiwa napita; natarajia kuwa na muda wa kutosha wa kukaa nanyi, kama Bwana akiruhusu. 8Lakini nitakaa Efeso mpaka wakati wa Pentekoste. 9Kwa maana mlango umefunguliwa kwangu kufanya kazi yenye matunda, na huko kuna wapinzani wengi . 10Ikiwa Timotheo atakuja kwenu mkaribisheni asiwe na woga wo wote akiwa nanyi kwa sababu anaendeleza kazi ya Bwana, kama mimi nifanyavyo. 11Basi asiwepo mtu atakayemdharau. Msafirisheni kwa amani ili aweze kunirudia. Namtegemea yeye pamoja na hao ndugu.

12Na sasa, kuhusu ndugu yetu Apolo. Nilimsihi sana awa tembelee pamoja na wale ndugu wengine, lakini haikuwa mapenzi yake kuja huko wakati huu. Atakuja apatapo nafasi.

Maneno Ya Mwisho

13Kesheni; simameni imara katika imani, muwe shujaa na hodari. 14Fanyeni kila kitu katika upendo. 15Sasa ndugu zangu, mnafahamu kwamba watu wa nyumbani kwa Stefana walikuwa waamini wa kwanza katika Akaya, nao wamejitoa kuwasaidia watu wa Mungu. 16Nawasihi mnyenyekee na kufuata uongozi wa watu kama hawa, na wa kila mtendakazi mwenzenu na kila anayejibidisha katika kazi. 17Nilifurahi wakati Stefana, Fortunato na Akaiko walipofika, kwa maana hawa wamenisaidia yale niliyopungukiwa kutoka kwenu. 18Wao wameburudisha roho yangu na yenu pia. Watu kama hawa, wanastahili kutambuliwa. 19Makanisa ya Asia wanawas alimu. Akila na Priska, pamoja na kanisa lililoko nyumbani kwao wanawasalimu katika Bwana. 20Pia ndugu wote wanawasalimu. Sali mianeni kwa busu takatifu. 21Mimi Paulo, kwa mkono wangu mwe nyewe, naandika salamu hii. 22Kama mtu ye yote hampendi Bwana, na alaaniwe. ‘Maranatha.’ Bwana wetu, njoo! 23Neema ya Bwana Yesu iwe nanyi.