1 Wakorintho 8

Chakula Kilichotolewa Sadaka Kwa Sanamu

1Sasa kuhusu chakula kilichotolewa sadaka kwa sanamu. Tuna jua kwamba ‘sisi sote tuna ujuzi.’ Lakini ‘ujuzi’ huleta maji vuno, ila upendo hujenga. 2Mtu anayedhania kwamba anajua kitu, basi hajafahamu kama inavyompasa kujua. 3Lakini kama mtu anam penda Mungu, mtu huyo anajulikana na Mungu.

4Kwa hiyo basi, kuhusu kula chakula kilichotolewa sadaka kwa sanamu: tunajua kwamba ‘sanamu haina uhai wa kweli’ na kwamba ‘kuna Mungu mmoja tu.’ 5Kwa maana hata kama wapo hao wanaoitwa ‘miungu,’ kama ni mbinguni au duniani; na kwa kweli wapo ‘miungu’ wengi na ‘mabwana’ wengi; 6sisi tunajua kwamba kuna Mungu mmoja, aliye Baba, ambaye vitu vyote vinatoka kwake, na sisi tunaishi kwa ajili yake; na kuna Bwana mmoja, Yesu Kristo, ambaye vitu vyote vimekuwepo kupitia kwake na tunaishi kutokana naye.

7Lakini si wote wanajua mambo haya. Watu wengine mpaka leo bado wamezoea miungu ya sanamu kiasi ambacho wanapokula chakula hicho wanadhani ni chakula kilichotolewa kwa sanamu, na kwa kuwa dhamiri yao ni dhaifu, inadhurika. 8Lakini chakula hakitusaidii kuwa karibu zaidi na Mungu. Hatupotezi cho chote tusipokula, wala hatupati faida yo yote kama tukila.

9Lakini hata hivyo tuwe waangalifu jinsi tunavyotumia uhuru wetu tusije tukawakwaza walio dhaifu katika imani. 10Kwa maana kama mtu mwenye dhamiri dhaifu akiwaona ninyi wenye ujuzi mkila katika hekalu la sanamu, je, si atavutwa kula chakula kilichoto lewa kwa sanamu? 11Kwa njia hiyo, huyo ndugu mwenye dhamiri dhaifu, ambaye Kristo alimfia, atateketea kwa sababu ya ujuzi wako. 12Mnapowatenda dhambi ndugu zenu kwa njia hii na kuharibu dhamiri zao dhaifu, mnamkosea Kristo. 13Kwa hiyo kama chakula kitamfanya ndugu yangu aanguke katika dhambi, sitakula nyama kamwe, nisije nikamfanya ndugu yangu aanguke.