1Kutoka kwa Petro, mtume wa Yesu Kristo. Kwa wateule wa Mungu ambao wametawanyika, wanaoishi ugenini huko Ponto, Galatia, Kapadokia, Asia na Bithinia. 2 Ninyi mlichaguliwa tangu mwanzo na Mungu Baba na kutakaswa na Roho, mpate kumtii Yesu Kristo na kunyunyiziwa damu yake. Nawatakieni neema na amani tele.
Tumaini Lenye Uzima
3 Asifiwe Mungu, Baba wa Bwana wetu Yesu Kristo! Kwa rehema yake kuu ametufanya tuzaliwe upya ili tupate tumaini lenye uzima kwa kufufuka kwa Bwana wetu Yesu Kristo kutoka kwa wafu; 4 na tupokee urithi usioharibika, usiooza na usiochuja, ambao umewekwa mbinguni kwa ajili yenu. 5 Nanyi, kwa imani, mnalindwa na nguvu ya Mungu mpaka utakapofika wokovu ambao uko tayari kufunuliwa wakati wa mwisho.
6 Furahini sana katika hilo, ingawa sasa kwa kitambo kidogo ni lazima mpate majaribu ya kila aina. 7 Majaribu yataifanya imani yenu, ambayo ina thamani kuliko dhahabu, iwe imepimwa na kuthibitishwa kuwa ya kweli kama vile dhahabu ambayo ingawa ni kitu kiharibikacho, hupimwa kwa moto. Ndipo mtapata sifa, utukufu na heshima siku ile Yesu Kristo atakapofunuliwa. 8 Ingawa hamja pata kumwona, mnampenda. Na ingawa hamumwoni sasa mnamwamini na kujawa na furaha tukufu isiyoelezeka. 9 Maana mnapokea wokovu wa roho zenu, ambao ndio lengo la imani yenu.
10 Manabii waliotabiri kuhusu neema hiyo ambayo ninyi mnge pewa, walitafuta sana na kwa makini habari za wokovu huu. 11 Walijaribu kutafuta kujua ni nani au ni wakati upi uliomaan ishwa na Roho wa Kristo aliyekuwa akisema ndani yao alipotabiri kuhusu mateso ya Kristo na utukufu utakaofuata. 12 Walidhihir ishiwa kuwa kazi waliyokuwa wakifanya si kwa faida yao bali ni kwa ajili yenu. Kwa maana walinena nanyi habari za mambo ambayo sasa mmekwisha elezwa na wale waliowahubiria Injili kwa uwezo wa Roho Mtakatifu aliyetumwa kutoka mbinguni. Hata malaika wanata mani kufahamu mambo haya.
Mwito Wa Kuishi Maisha Matakatifu
13 Kwa hiyo, ziandaeni nia zenu, muwe na kiasi, wekeni tumaini lenu lote katika neema ile mtakayopewa wakati ule Yesu Kristo atakapodhihirishwa. 14 Kama watoto watiifu, msikubali kutawaliwa na tamaa mbaya mlizokuwa nazo wakati mkiishi katika ujinga. 15 Bali kama yeye aliyewaita alivyo mtakatifu, kadhalika ninyi muwe watakatifu katika mwenendo wenu; 16 maana imeandikwa: “Muwe watakatifu kwa sababu mimi ni mtakatifu.”
17 Kwa kuwa mnamwita “Baba” yeye ahukumuye matendo ya kila mtu pasipo upendeleo, ishini maisha yenu hapa duniani kama wageni, kwa kumcha Mungu. 18 Maana mnafahamu kwamba mlikombolewa kutokana na maisha duni yasiyofaa ambayo mlirithi kutoka kwa baba zenu. Hamkukombolewa kwa kutumia vitu viharibikavyo kama fedha na dhahabu, 19 bali mlikombolewa kwa damu ya thamani ya Kristo, Mwana-Kondoo asiye na dosari wala doa. 20 Yeye alichaguliwa kabla ya dunia kuumbwa lakini akadhihirishwa katika siku hizi za mwisho kwa ajili yenu. 21 Kwa ajili yake ninyi mnamwamini Mungu aliyemfufua kutoka kwa wafu akampa utukufu, na kwa hiyo imani yenu na matumaini yenu yako kwa Mungu.
22 Na sasa kwa kuwa mmekwisha kujitakasa kwa kuitii ile kweli na kuwapenda ndugu zenu kwa kweli, pendaneni kwa moyo wote. 23 Maana mmezaliwa upya, si kwa mbegu iharibikayo, bali kwa mbegu isiyoharibika, kwa neno la Mungu lililo hai na linalodumu hata milele. 24 Maana, “Binadamu wote ni kama nyasi na utukufu wao ni kama ua la mwituni. Nyasi hunyauka na ua huanguka, 25 lakini neno la Mungu hudumu milele.” Na neno hilo ni Habari Njema ambayo mlihubiriwa.