Wafilipi 2

Unyenyekevu Na Ukuu Wa Kristo

1Ikiwa mmepata faraja kwa kuwa mmeunganishwa na Kristo, kama mmevutwa na upendo wake na kushiriki Roho wake, kama mnaoneana huruma na kusaidiana; basi kamilisheni furaha yangu kwa kuwa na nia moja, upendo mmoja na kuwa wamoja katika roho na shabaha. Msifanye jambo lo lote kwa ajili ya ubinafsi au kwa kujiona, bali kuweni wanyenyekevu, mkiwahesabu wengine kuwa bora kuliko ninyi. Kila mtu asiangalie mambo yake mwenyewe, bali kila mtu ajishughulishe pia kwa faida ya wengine. Muwe na nia kama ile aliyokuwa nayo Kristo Yesu; yeye kwa asili alikuwa sawa na Mungu, lakini hakuona kwamba kuwa sawa na Mungu ni kitu cha kush ikilia sana. Bali alikubali kuacha vyote, akachukua hali ya mtumishi, akazaliwa na umbo la wanadamu. Alipochukua umbo la mwanadamu, alijinyenyekeza akawa mtii mpaka kufa, tena kifo cha msalaba. Kwa sababu hiyo, Mungu alimwinua juu kabisa, akampa jina ambalo ni kuu kuliko majina yote; 10 ili kwa jina la Yesu, kila goti lipigwe, mbinguni na duniani na kuzimu; 11 na kila ulimi ukiri kwamba Yesu Kristo ni Bwana, kwa utukufu wa Mungu

Ng’aeni Kama Nyota

12 Basi rafiki zangu wapendwa, kama ambavyo mmekuwa mkitii nilipokuwa nanyi, nawasihi mwendelee kunitii vivyo hivyo, na hata zaidi sasa kwa kuwa sipo pamoja nanyi. Endeleeni kufanya bidii kwa ajili ya wokovu wenu huku mkitetemeka na kuogopa. 13 Kwa maana ni Mungu ambaye anatenda kazi ndani yenu, akiwapa nia ya kutimiza mapenzi yake na kuwawezesha kutenda yale yanayompendeza 14 Fanyeni mambo yote bila manung’uniko au mabishano 15 ili msiwe na lawama au kosa bali muwe wana wa Mungu wasio na kasoro katika ulimwengu uliopotoka, mking’aa kama nyota angani, 16 na kusisitiza neno la uzima. Mkifanya hivyo siku ya Kristo nitajisi fia kwamba sikupiga mbio au kufanya kazi bure. 17 Hata kama damu yangu itamwagwa kama sadaka juu ya dhabihu na huduma inayotokana na imani yenu, mimi ninafurahi na kushangilia pamoja nanyi nyote. 18 Vivyo hivyo, nanyi pia mnapaswa kufurahi na kushangilia pamoja nami.

Safari Ya Timotheo Na Epafrodita

19 Nina matumaini katika Bwana Yesu ya kumtuma Timotheo hivi karibuni aje kwenu, ili nipate habari za kunitia moyo kutoka kwenu. 20 Sina mtu mwingine hapa kama yeye, anayewatakieni mema kwa moyo wote. 21 Wengine wanajishughulisha zaidi na mambo yao wenyewe na hawajali lo lote kuhusu kazi ya Yesu Kristo. 22 Lakini ninyi wenyewe mnajua jinsi Timotheo alivyojithibit isha, kwa maana amefanya kazi ya Injili pamoja nami kama vile mtoto na baba yake. 23 Kwa hiyo, natumaini kumtuma Timotheo kwenu mara tu nipatapo habari kuhusu mambo yangu yatakavyokuwa. 24 Nami naamini katika Bwana kwamba mimi mwenyewe nitakuja kwenu hivi karibuni.

25 Nimeona vema kumrudisha ndugu yangu Epafrodita kwenu. Yeye ni mtumishi na askari mwenzangu, ambaye pia ni mjumbe wenu mliyemtuma anihudumie katika mahitaji yangu. 26 Yeye ana hamu kuwaoneni ninyi nyote, na amesikitishwa kwa sababu mlipata habari kwamba alikuwa mgonjwa. 27 Hakika alikuwa mgonjwa, tena karibu ya kufa. Lakini Mungu alimhurumia, na si yeye tu, bali hata na mimi alinihurumia, nisipatwe na huzuni juu ya huzuni . 28 Kwa hiyo napenda kumtuma kwenu ili mtakapomwona kwa mara nyingine, mpate kufurahi, na mimi nipunguziwe wasiwasi wangu. 29 Kwa hiyo mpokeeni katika Bwana kwa furaha kubwa; na wapeni heshima watu kama hawa. 30 Kwa maana alikaribia kufa kwa ajili ya kazi ya Kristo; alihatarisha maisha yake ili aweze kunipa msaada ambao ninyi msingeweza kunipa.