Kutoa Kwa Ukarimu
1Tunapenda mfahamu ndugu zetu, kuhusu neema ambayo Mungu amewapa makanisa ya Makedonia. 2 Pamoja na majaribu makali na taabu walizopata, furaha yao na umaskini wao mkuu zimezaa utajiri wa ukarimu. 3 Ninashuhudia kwamba walitoa kwa kadiri ya uwezo wao hata na zaidi ya uwezo wao. 4 Kwa hiari yao wenyewe, walitusihi wapewe nafasi ya kushiriki katika huduma hii ya kuwasaidia watu wa Mungu. 5 Na hawakufanya tulivyotazamia bali walijitoa wao wenyewe kwa Bwana kwanza na ndipo wakajitoa kwetu, kufuatana na mapenzi ya Mungu. 6 Kwa hiyo tulimwagiza Tito, kwa kuwa ndiye aliyeanzisha jambo hili, akamilishe kazi hii ya neema pia kwa upande wenu. 7 Basi, kama mlivyo mbele sana katika yote: katika imani, katika kutamka, katika juhudi na katika kutupenda, hakik isheni kuwa mnakuwa wa kwanza pia katika neema hii ya kutoa.
8 Siwapi amri, lakini nawaonyesha jinsi wengine walivyo tay ari kutoa ili kupima ukweli wa upendo wenu. 9 Kwa maana mnajua neema ya Bwana wetu Yesu Kristo, ambaye ingawa alikuwa tajiri, alikubali kuwa maskini kwa ajili yenu, ili kwa umaskini wake ninyi mpate kuwa matajiri. 10 Ushauri wangu kuhusu jambo hili ni huu. Ni vyema mkamilishe sasa jambo ambalo mlinia na mkaanza kulifanya tangu mwaka jana 11 ili wepesi wenu katika kunia ulin gane na kumaliza kwenu kutoa kwa kadiri ya mlicho nacho. 12 Kwa kuwa kama nia ya kutoa ipo, kitolewacho kinakubalika kufuatana na kile mtu alicho nacho, si kufuatana na kile ambacho mtu hana. 13 Nia yetu si kwamba wengine wasaidike wakati ninyi mnateseka bali pawe na uwiano. 14 Kwa wakati huu wingi wa vitu mlivyonavyo usaidie kutosheleza mahitaji yao, ili wakati wao wakiwa na wingi wa vitu, nao wapate kutosheleza mahitaji yenu. 15 Ndipo patakuwa na usawa, kama maandiko yanavyosema, “Aliyekusanya kwa wingi, hakubakiza kitu, na aliyekusanya kidogo hakupungukiwa.”
Tito Anatumwa Korintho
16 Tunamshukuru Mungu ambaye amempa Tito moyo wa kuwajali ninyi kama mimi ninavyowajali. 17 Si kwamba amekubali ombi letu tu, bali anakuja kwenu akiwa na ari na kwa hiari yake mwenyewe. 18 Pamoja naye tunamtuma ndugu ambaye anasifiwa na makanisa yote kwa huduma yake ya kuhubiri Injili. 19 Zaidi ya hayo, amechagu liwa na makanisa asafiri nasi kupeleka matoleo haya. Hii ni huduma ambayo tunafanya kwa utukufu wa Bwana na pia kuonyesha nia yetu ya kuwasaidia wengine. 20 Tumenuia kwamba mtu ye yote asiwe na sababu ya kutulaumu kuhusu jinsi tunavyosima mia matoleo haya ya ukarimu. 21 Tunajitahidi kuhakikisha kuwa tunafanya haki machoni pa Bwana na machoni penu, na wala si kama sisi tuonavyo vyema. 22 Pamoja na hawa, tunamtuma ndugu yetu ambaye tumempima mara nyingi tukamwona kuwa wa kweli na mwenye juhudi, hasa zaidi sana kwa kuwa ana imani kubwa kwenu. 23 Kumhusu Tito, yeye ni mwenzangu na mfanyakazi pamoja nami kwa ajili yenu. Kuhusu hawa ndugu wengine, wao ni wawakilishi wa makanisa, nao wanamletea Kristo utukufu. 24 Kwa hiyo, waonyesheni hawa ndugu upendo wenu na sababu inayotufanya tujivune kwa ajili yenu, ili makanisa yote yapate kuona.