Waebrania 10

Dhabihu Ya Kristo Ilikuwa Ya Mwisho

1Basi kwa kuwa sheria ni kivuli tu cha mambo mema yajayo na wala si mambo yenyewe, haiwezi kamwe, kwa njia ya dhabihu zito lewazo mwaka hadi mwaka, kuwakamilisha wale wanaoabudu. 2Kama isingekuwa hivyo, dhabihu hizo zingekuwa hazitolewi tena. Maana hao waabuduo wasingalijiona tena kuwa wana hatia kwa ajili ya dhambi zao baada ya kutakaswa mara moja. 3Badala yake, dhabihu hizo zilikuwa ni ukumbusho wa dhambi mwaka hadi mwaka. 4Kwa maana damu ya mafahali na mbuzi, haiwezi kamwe kuondoa dhambi.

5Kwa sababu hii, Yesu alipokuja duniani alisema: “Hukutaka dhabihu na sadaka bali umeniandalia mwili. 6Hukupendezwa na sadaka za kuteketezwa wala sadaka zitolewazo kwa ajili ya dhambi. 7Ndipo nikasema, ‘Nipo hapa, kama ilivyoandikwa katika gombo la sheria kunihusu; nimekuja kutimiza mapenzi yako wewe Mungu.’ ”

8Kwanza alisema, “Dhabihu na sadaka, sadaka za kuteketezwa wala sadaka zitolewazo kwa ajili ya dhambi hukutaka, wala huku pendezwa nazo,” ingawa hizi zilitolewa kwa mujibu wa sheria. 9Kisha akasema, “Niko hapa, nimekuja kutimiza mapenzi yako.” Anaweka kando ule utaratibu wa kwanza na kuanzisha utaratibu wa pili. 10Na kwa mapenzi hayo, sisi tumetakaswa kwa njia ya sadaka ya mwili wa Yesu Kristo alioutoa mara moja tu, kwa wakati wote.

11Kila kuhani husimama siku hadi siku akifanya huduma yake ya ibada na akitoa tena na tena dhabihu zile zile ambazo haziwezi kuondoa dhambi. 12Lakini Kristo alipokwisha kutoa dhabihu yake kwa ajili ya dhambi mara moja tu kwa wakati wote, aliketi upande wa kulia wa Mungu. 13Tangu wakati huo anangoja mpaka Mungu atakapowafanya maadui zake kuwa kiti cha miguu yake. 14Maana kwa dhabihu moja tu amewafanya kuwa wakamilifu milele wale wote wanaotakaswa.

15Roho Mtakatifu pia anatushuhudia kuhusu jambo hili. Kwanza anasema: 16“Hili ndilo agano nitakalofanya nao baada ya siku hizo, asema Bwana. Nitaziweka sheria zangu mioyoni mwao na kuziandika akilini mwao.” 17Kisha anasema: “Dhambi zao na makosa yao sitayakumbuka tena kamwe.”

18Basi, haya yakishasamehewa, hakuna tena dhabihu inayoto lewa kwa ajili ya dhambi.

Haja Ya Kuwa Imara

19Kwa hiyo ndugu zangu, kwa kuwa tunao ujasiri wa kuingia Patakatifu pa Patakatifu kwa damu ya Yesu, 20kwa njia mpya iliyo hai tuliyofunguliwa kupitia lile pazia, yaani kwa njia ya mwili wake, 21na kwa kuwa tunaye kuhani mkuu anayemiliki nyumba ya Mungu; 22basi tumkaribie Mungu kwa moyo wa kweli na imani timilifu, mioyo yetu ikiwa imenyunyizwa na kuwa safi kutokana na dhamiri mbaya na miili yetu ikiwa imeoshwa kwa maji safi. 23Tushikilie kwa makini tumaini tunalokiri kwa maana yeye ali yeahidi ni mwaminifu. 24Na tujishughulishe kutafuta jinsi ya kuhimizana katika kuonyeshana upendo na kutenda mema. 25Tusiache kukutana pamoja, kama wengine wanavyofanya, bali tutiane moyo, hasa zaidi tunapoona siku ile ikikaribia.

Hatari Ya Kukufuru

26Kama tukiendelea kutenda dhambi makusudi baada ya kupokea na kufahamu ile kweli, hakuna tena dhabihu iliyobaki inayoweza kutolewa kwa ajili ya dhambi. 27Kinachobakia ni kungojea kwa hofu hukumu ya Mungu na moto mkali utakaowaangamiza maadui zake. 28Mtu aliyevunja sheria ya Mose aliuawa pasipo huruma kwa usha hidi wa watu wawili au watatu. 29Je, mnadhani ni adhabu kali kiasi gani zaidi anastahili kupewa mtu ambaye anamdharau na kum kataa Mwana wa Mungu, na ambaye anaona kuwa damu ya agano iliyom takasa si kitu, na ambaye amemtukana Roho wa neema? 30Kwa maana tunamjua yeye aliyesema, “Kulipiza kisasi ni juu yangu, mimi nitalipiza.” Pia alisema, “Bwana atawahukumu watu wake.” 31Kuanguka mikononi mwa Mungu aliye hai ni jambo la kutisha.

32Kumbuka siku zile za mwanzo baada ya kupokea mwanga, jinsi mlivyovumilia mapambano makali na mateso. 33Wakati mwin gine mlitukanwa na kuteswa hadharani; wakati mwingine mlikuwa radhi kuungana na wale walioteswa hivyo. 34Mliwaonea huruma waliokuwa kifungoni, na mkakubali kwa furaha kunyang’anywa mali zenu kwa maana mlifahamu kwamba mlikuwa na mali bora zaidi inay odumu.

35Kwa hiyo msitupe tumaini lenu, ambalo litapewa tuzo kubwa. 36Mnahitaji kuvumilia ili mkisha kufanya mapenzi ya Mungu mpate kile alichoahidi. 37“Kwa kuwa bado kitambo kidogo tu yeye anayekuja atakuja , wala hatakawia; 38lakini mtu wangu mwenye haki ataishi kwa imani, na akirudi nyuma sitapendezwa naye.”

39Lakini sisi hatumo miongoni mwa hao wanaorudi nyuma wakaangamizwa, bali sisi ni miongoni mwa wanaoamini wakaokolewa.