Waefeso 5

1Kwa hiyo mfuateni Mungu kama watoto wapendwa. 2Muishi maisha ya upendo kama Kristo alivyotupenda sisi akajitoa kwa ajili yetu kuwa sadaka yenye harufu nzuri na dhabihu kwa Mungu. 3Lakini uasherati, uchafu wa aina zote na tamaa, wala yasitajwe miongoni mwenu, kwa maana mambo haya hayawastahili watakatifu wa Mungu. 4Kusiwepo na mazungumzo machafu ya aibu, au maneno ya upuuzi au mzaha; mazungumzo ya namna hii hayafai. Badala yake mshukuruni Mungu. 5Mjue hakika kwamba hakuna mwasherati wala mtu mwenye mawazo machafu, wala mwenye tamaa, yaani mwabudu sanamu, ambaye ataurithi Ufalme wa Kristo na wa Mungu. 6Msikubali kudan ganywa na mtu ye yote kwa maneno matupu, kwa kuwa hasira ya Mungu huwaka kwa sababu ya mambo kama haya juu ya watu wote wasiomtii. 7Kwa hiyo, msishirikiane nao. 8Zamani ninyi pia mlikuwa gizani, lakini sasa mmekuwa nuru katika Bwana; basi muishi kama watoto wa nuru. 9Kwa maana tunda la nuru hupatikana katika kila lililo jema, lililo la haki na la kweli. 10Jifunzeni mambo yanayom pendeza Bwana. 11Msishiriki matendo ya giza yasiyofa a, bali yafichueni. 12Kwa maana ni aibu hata kutaja mambo wanayofanya kwa siri. 13Lakini ikiwa jambo lo lote linawekwa katika nuru, huonekana, kwa maana ni nuru inayofanya vitu vionekane. 14Ndio sababu husemwa, “Amka wewe uliyelala, ufufuke kutoka kwa wafu, na Kristo atakuangazia.” 15Kwa hiyo muwe waangalifu jinsi mnavyoishi; msiishi kama watu wasio na hekima, bali kama watu wenye hekima, 16mkitumia vizuri muda mlio nao, kwa maana hizi ni nyakati za uovu. 17Kwa hiyo msiwe wajinga, bali muelewe yaliyo mapenzi ya Mungu. 18Pia msilewe divai, kwa sababu huo ni upotovu, bali mjazwe Roho. 19Zungumzeni ninyi kwa ninyi kwa zaburi na nyimbo na tenzi za rohoni, mkimwimbia Mungu mioyoni mwenu kwa sauti tamu. 20Wakati wote na kwa kila kitu mshukuruni Mungu Baba katika jina la Bwana wetu Yesu Kristo. 21Kila mmoja wenu ajinyenyekeze kwa mwenzake kwa sababu ya upendo mlio nao kwa Kristo. 22Wake, watiini waume zenu kama mnavyomtii Bwana. 23Kwa maana mume ni kichwa cha mke kama vile Kristo alivyo kichwa cha kanisa, ambalo ni mwili wake, naye mwe nyewe ni Mwokozi wa kanisa. 24Basi, kama vile Kanisa linavyom tii Kristo, vivyo hivyo na wake pia wanapaswa kuwatii waume zao kwa kila jambo. 25Ninyi waume, wapendeni wake zenu, kama Kristo alivyolipenda kanisa akajitoa nafsi yake kwa ajili yake ili 26alitakase. Alifanya hivyo kwa kuliosha kwa maji na kwa neno lake 27ili ajipatie kanisa linalong’aa, lisilo na doa wala kunjamano wala kitu kingine cho chote kama hicho; liwe takatifu na bila kasoro. 28Vivyo hivyo waume wawapende wake zao kama miili yao. Anayempenda mkewe anajipenda mwenyewe. 29Hakuna mtu anayeuchukia mwili wake mwenyewe, bali huulisha na kuutunza vizuri, kama Kristo anavyolitunza kanisa lake. 30Sisi tu viungo vya mwili wake. 31“Kwa sababu hii, mwanaume atamwacha baba yake na mama yake, naye ataungana na mkewe, na hawa wawili wata kuwa mwili mmoja.” 32Hili ni fumbo gumu kueleweka, nami nasema kuwa ni kielelezo kuhusu Kristo na kanisa. 33Hata hivyo kila mmoja wenu ampende mkewe kama anavyoipenda nafsi yake; na mke naye ahakikishe anamheshimu mumewe. Watoto Na Wazazi