Kuwa Na Amani Na Mungu
1Basi, kwa kuwa tumekwisha kuhesabiwa haki kwa imani, tuna amani na Mungu kwa ajili ya Bwana wetu Yesu Kristo. 2Kwa kupitia kwake tumepata njia ya kufikia neema hii ambayo inatuwezesha kusimama imara, tukifurahia tumaini letu la kushiriki utukufu wa Mungu. 3Zaidi ya hayo, pia tunafurahia mateso yetu kwa sababu tunafahamu kuwa mateso huleta subira; 4na subira huleta uthabiti wa moyo; na uthabiti wa moyo hujenga tumaini. 5Tukiwa na tumaini hatuwezi kukata tamaa kwa sababu Mungu amekwisha kumimina upendo wake mioyoni mwetu kwa njia ya Roho Mtakatifu ambaye ni zawadi tuliyopewa na Mungu.
6Tulipokuwa tungali wanyonge, wakati aliochagua Mungu, Kristo aliwafia wenye dhambi. 7Ni vigumu sana kwa mtu kujitolea kufa kwa ajili ya mwenye haki, ingawa yawezekana mtu akajitolea kufa kwa ajili ya mtu mwema. 8Lakini Mungu anaudhihirisha upendo wake kwetu kwamba: tulipokuwa tungali wenye dhambi, Kristo ali kufa kwa ajili yetu.
9Basi, kwa kuwa tumekwisha kuhesabiwa haki kwa damu yake, bila shaka atatuokoa kutoka katika ghadhabu ya Mungu. 10Kwa kuwa kama tulipokuwa maadui wa Mungu tulipatanishwa kwa kifo cha Mwanae, bila shaka sasa kwa kuwa tumepatanishwa, tutaokolewa kwa uzima wake. 11Si hivyo tu, bali pia tunamfurahia Mungu katika Bwana wetu Yesu Kristo ambaye kwa ajili yake tumepokea upatanisho wetu.
Adamu Alileta Kifo, Yesu Ameleta Uzima
12Kwa hiyo kama vile ambavyo dhambi iliingia ulimwenguni kupitia kwa mtu mmoja, na dhambi ikaleta kifo, na kwa njia hiyo kifo kikawajia watu wote kwa kuwa wote walitenda dhambi -
13kwa maana kabla sheria haijatolewa dhambi ilikuwepo ulimwenguni. Lakini dhambi haihesabiwi ambapo hakuna sheria. 14Hata hivyo tangu wakati wa Adamu hadi wakati wa Musa, kifo kiliwatawala watuwote hata wale ambao dhambi zao hazikuwa kama uasi wa Adamu. Adamu alikuwa mfano wa yule ambaye angalikuja. 15Lakini zawadi iliyotolewa bure haiwezi kulinganishwa na ule uasi. Kwa maana ikiwa watu wengi walikufa kwa sababu ya uasi wa mtu mmoja, basi neema ya Mungu na zawadi iliyotolewa kwa ajili ya mtu mmoja, Yesu Kristo, imemiminika kwa wingi zaidi kwa watu wengi. 16Pia zawadi ya Mungu sio kama matukio ya ile dhambi ya mtu mmoja. Kwa maana hukumu iliyotokana na uasi huo ilileta laana, lakini zawadi iliyopatikana bure baada ya dhambi nyingi, inaleta haki ya Mungu. 17Na ikiwa kutokana na uasi wa mtu mmoja kifo kilitawala kupitia huyo mtu mmoja, wale wanaopokea wingi wa neema na zawadi ya bure ya kuhesabiwa haki, watatawala zaidi sana katika maisha kwa ajili ya huyo mtu mmoja, Yesu Kristo. 18Kwa hiyo, kama vile uasi wa mtu mmoja ulivyoleta hukumu kwa watu wote, hali kadhalika, tendo la haki la mtu mmoja linawafanya watu wote waachiliwe huru na kupewa uzima. 19Na kama vile ambavyo watu wengi walifanywa kuwa wenye dhambi kwa ajili ya kutokutii kwa mtu mmoja, vivyo hivyo wengi watahesabiwa haki na Mungu kwa ajili ya utii wa mtu mmoja.
20Sheria ililetwa ili dhambi iongezeke. Lakini dhambi ili poongezeka, neema iliongezeka zaidi. 21Kama vile ambavyo dhambi ilitawala kwa njia ya kifo, vivyo hivyo neema ya Mungu iweze kutawala kwa njia ya haki, ikileta uzima wa milele katika Yesu