Maagizo Kwa Timotheo
1Roho anasema wazi wazi kwamba katika siku za mwisho watu wengine wataiacha imani yao na kusikiliza roho za udanganyifu na mafundisho ya mashetani. 2Mafundisho hayo yanaletwa na wanafiki waongo ambao dhamiri zao zimekufa kama vile zimechomwa kwa chuma cha moto. 3Wao wanawazuia watu kuoa; na wanawaamrisha watu wasile vyakula vya aina fulani - ambavyo Mungu aliviumba vipoke lewe kwa shukrani na wale wanaoamini na waliopata kuijua kweli. 4Kwa maana kila kitu alichokiumba Mungu ni chema wala kitu cho chote kisikataliwe kama kinapokelewa kwa shukrani, 5maana kina takaswa kwa neno la Mungu na kwa sala.
Mtumishi Mwema Wa Kristo
6Ukiwapa ndugu mafundisho haya, utakuwa mtumishi mwema wa Kristo Yesu ambaye amelishwa vema kwa maneno ya imani na yale mafundisho mema uliyoyafuata. 7Usijishughulishe kabisa na hadithi zisizo za kidini ambazo hazina maana. Jizoeze kuishi kwa kumcha Mungu. 8Maana japokuwa mazoezi ya mwili yana faida kiasi, kumcha Mungu kuna faida kwa kila hali, kwa sababu kumcha Mungu kuna faida kwa maisha ya sasa na maisha yajayo.
9Neno hili ni la kweli na linastahili kupokelewa, 10na kwa ajili yake sisi tunajitahidi na kutaabika, kwamba tumeweka tumaini letu kwa Mungu aliye hai, ambaye ni Mwokozi wa watu wote, hasa wale waaminio.
11Agiza na kufundisha mambo haya. 12Mtu asikudharau kwa kuwa wewe ni kijana, bali uwe mfano mwema kwa waamini wote kwa maneno yako, kwa mwenendo wako, katika upendo, imani na usafi.
13Mpaka hapo nitakapokuja, tumia wakati wako katika kusoma Maandiko hadharani, kuhubiri, na kufundisha. 14Usiache kutumia kipawa ulichonacho, ambacho ulipewa kwa neno la unabii wakati wazee wa kanisa walipokuwekea mikono. 15Tekeleza mambo haya. Tumia nguvu zako na wakati wako kuyatimiza ili watu wote waone maendeleo yako.
16Jilinde sana, na utunze mafundisho yako. Yashikilie, maana kwa kufanya hivyo utajiokoa wewe mwenyewe na wale wanaoku sikiliza.