1 Timotheo 2

Maagizo Kuhusu Ibada

1Basi, kwanza kabisa, naagiza kwamba dua, sala, maombezi na shukrani zitolewe kwa ajili ya watu wote: 2kwa ajili ya wafalme na wote wenye mamlaka, ili tupate kuishi maisha ya utulivu na amani, tukimcha Mungu na kuwa wenye heshima kwa kila njia. 3Jambo hili ni jema na linampendeza Mungu Mwokozi wetu 4ambaye anapenda watu wote waokolewe na wapate kuijua kweli. 5Maana kuna Mungu mmoja na mpatanishi mmoja kati ya Mungu na wanadamu, yaani mwanadamu Kristo Yesu, 6aliyejitoa mwenyewe kuwa fidia kwa ajili ya wote. Yeye ni uthibitisho wa mambo haya, uliotolewa kwa wakati wake. 7Na hii ndio sababu nilichaguliwa niwe mhubiri na mtume, nasema kweli sisemi uwongo; nilichaguliwa niwe mwalimu wa watu wa mataifa katika imani na kweli.

8Kwa hiyo, nataka kila mahali wanaume wasali wakiinua mikono iliyotakaswa pasipo hasira wala mabishano. 9Kadhalika, nataka wanawake wajipambe kwa heshima na kwa busara. Mavazi yao yawe nadhifu, si kwa kusuka nywele, kujipamba kwa dhahabu, lulu na mavazi ya gharama kubwa, 10bali kwa matendo mema kama iwapa savyo wanawake wanaokiri kuwa wanamcha Mungu. 11Mwanamke na ajifunze katika utulivu na unyenyekevu.

12Simruhusu mwanamke ye yote kufundisha au kuwa na mamlaka juu ya wanaume. Mwanamke anapaswa kukaa kimya. 13Kwa maana Adamu aliumbwa kwanza kisha Hawa; 14na Adamu hakudanganywa bali mwanamke alidanganywa akawa mkosaji. 15Lakini mwanamke ataoko lewa kwa kuzaa, kama ataendelea kudumu katika imani, upendo na utakatifu, pamoja na kujiheshimu.