2 Timotheo 3

Hatari Za Siku Za Mwisho

1Lakini fahamu jambo hili: kwamba siku za mwisho kutakuwa na nyakati za taabu. 2Maana watu watakuwa wenye kujipenda wenyewe, wenye kupenda fedha, wenye kujisifu, wenye kiburi, watukanaji, wasiotii wazazi wao, wasio na shukrani, wasio na utakatifu; 3wasio na ubinadamu, wasiopenda kusuluhishwa, wachonganishi, walafi, wakatili, wasiopenda mema; 4wasaliti, wasiojali kitu, waliojaa majivuno, wapendao anasa badala ya kumpenda Mungu. 5Hao ni watu ambao kwa nje wataonekana kuwa wana dini, huku wakikana nguvu ya imani yao. Jiepushe na watu wa jinsi hiyo.

6Maana miongoni mwao wamo wale waendao katika nyumba za watu na kuwateka wanawake dhaifu waliolemewa na dhambi na kuyumbishwa na tamaa za kila namna. 7Wao humsikiliza kila mtu lakini hawawezi kutambua kweli. 8Kama vile Yane na Yambre walivyopin gana na Musa, kadhalika watu hawa nao wanapingana na ile kweli. Ni watu wenye akili potofu, wenye imani ya bandia. 9Lakini hawa tafika mbali, kwa sababu ujinga wao utakuwa dhahiri kwa watu wote, kama ulivyokuwa dhahiri ujinga wa hao watu wawili.

Maagizo Ya Paulo Kwa Timotheo

10Bali wewe umeyafahamu mafundisho yangu, mwenendo wangu, makusudio yangu, imani yangu, uvumilivu wangu, upendo wangu, ustahimilivu wangu, 11mateso yangu, taabu zangu. Umefahamu yote yaliyonipata huko Antiokia, Ikonia na Listra, mateso yote niliyostahimili; lakini Bwana aliniokoa katika hayo yote. 12Naam, na wote wapendao kuishi maisha ya kumcha Mungu ndani ya Kristo Yesu watateswa. 13Lakini watu waovu na wadanganyifu watazidi kuwa waovu, wakidanganya na kudanganyika. 14Bali wewe, udumu katika yale uliyojifunza na kuyaamini kwa uthabiti, ukitam bua umejifunza hayo kutoka kwa nani; 15na jinsi ambavyo tangu utoto wako umeyafahamu Maandiko matakatifu ambayo yanaweza kukuelekeza kupokea wokovu kwa kumwamini Kristo Yesu. 16Andiko zima lina pumzi ya Mungu nalo lafaa kwa mafundisho, kwa kuwaonya watu makosa yao, kuwaongoza na kuwafundisha katika haki 17ili mtu wa Mungu awe kamili akiwa na nyenzo zote za kutenda kila jambo jema.