Tito 2

Mafundisho Sahihi

1Lakini wewe, mafundisho yako ni lazima yawe sahihi. 2Wafundishe wazee kuwa na kiasi, watulivu, wenye busara na tha biti katika imani, upendo na subira. 3Hali kadhalika akina mama wazee wawe na mwenendo wa unyenyekevu. Wasiwe wachonganishi, wala wasiwe watumwa wa pombe; bali waonyeshe mfano mwema. 4Hivyo wawafundishe akina mama vijana kuwapenda waume zao na watoto wao 5na kuwa wenye kiasi na safi, wakitumia wakati wao kushughulika nyumbani mwao. Wawe wema na watii kwa waume zao, ili neno la Mungu lisije likadharauliwa kwa ajili yao. 6Vile vile uwahimize vijana kuwa na kiasi. 7Katika mambo yote wewe mwenyewe uwe kielelezo cha matendo mema. Uonyeshe usa hihi na uthabiti katika mafundisho yako. 8Maneno yako yawe na kina na mantiki safi, mtu asiweze kuyatoa kasoro na hata yule anayepinga aaibike kwa kukosa lo lote baya la kusema juu yetu.

9Wahimize watumwa kuwatii mabwana wao na kuwapendeza katika mambo yote; wasijibishane nao 10wala kuwaibia, bali watumwa waonyeshe kuwa wanaweza kuaminika kabisa ili katika kila hali mafundisho ya Mungu Mwokozi wetu yapate sifa njema.

11Kwa maana neema ya Mungu iletayo wokovu imedhihirishwa kwa watu wote. 12Neema hiyo inatufundisha kukataa uovu na tamaa za dhambi, tupate kuishi maisha ya kiasi, ya haki na ya kumcha Mungu, katika ulimwengu huu. Wakati huo huo 13tukingojea tumaini letu lenye baraka - kuja kwa utukufu wa Mungu wetu Mkuu na Mwokozi wetu, Yesu Kristo. 14Yeye alijitoa mwenyewe kwa ajili yetu ili atukomboe katika uasi wote, na kutufanya tuwe safi kwa ajili yake; na tuwe watu wake kabisa, ambao wana juhudi katika kutenda mema.

15Fundisha mambo haya; himiza na kemea kwa mamlaka yote. Mtu ye yote asikudharau.